Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo mgumu dhidi ya Simba SC huku akisisitiza kuwa hawapo tayari kuwa daraja la wapinzani wao katika mbio za ubingwa.
Akizungumza kuelekea mchezo huo utakaopigwa kwenye CCM Mkwakwani Stadium, Fikiri amesema maandalizi ya timu yamekuwa mazuri na benchi la ufundi limefanya uchambuzi wa kina wa mbinu za Simba ili kuandaa mkakati wa kukabiliana nao.
“Tunajua itakuwa mechi ngumu kwa sababu Simba wana malengo yao na sisi pia tuna malengo yetu. Hatutaki kuwa daraja la timu nyingine kupata pointi,” amesema Fikiri.
Kocha huyo amesema licha ya Simba kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji, Coastal Union nayo imejipanga vizuri defensively kuhakikisha inazuia mashambulizi yote ya wapinzani wao.

“Kikubwa kwetu hakuna presha. Wachezaji wamejipanga vizuri na wako tayari kupambana ili kupata ushindi,” ameongeza.
Hata hivyo, Fikiri amesema timu hiyo itawakosa wachezaji wawili, Abdallah Viva na James Msuva, kutokana na majeraha.
Kwa upande wake, nahodha wa Coastal Union, Jofrey Manyasi, amesema kikosi kiko tayari kwa mchezo huo na kinaamini kitatoa ushindani mkubwa dhidi ya Simba.
“Wachezaji wote wako tayari kwa mechi na tunaamini itakuwa mchezo mzuri,” amesema Manyasi.
Aidha, kocha huyo amewaomba mashabiki wa Coastal Union kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa timu sapoti katika mchezo huo muhimu.




