Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wote wanaodai fidia za kupisha miradi inayotekelezwa na Serikali, wanaendelea kulipwa na watalipwa.
Amesema hakuna mwananchi anayedai fidia halali, ambaye Serikali haitamlipa, muhimu ni kuwa na subira wakati mamlaka zinafanya tathmini kuhakiki madai hayo.
Dk Samia ametoa ahadi hiyo leo, Jumatatu Oktoba 13, 2025 alipozungumza na wananchi wa Geita Mjini, katika mkutano wa kampeni za urais, zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Amesema kwa wananchi wanaodai fidia kwa kupisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, zimeshaanza kulipwa na zitaendelea zitalipwa.
“Niwahakikishie wananchi wote wanaodai fidia zao, muwe na subira, tumeanza kulipa, tunaendelea kulipa na tutalipa kila fidia ambayo tunaihakiki na kuthibitisha kwamba ni madai ya kweli,” amesema.
Ameambatanisha ahadi hiyo na nasaha zake kwa wananchi wa Geita Mjini, akiwataka Oktoba 29, wajitokeze kwenda kupiga kura, huku mabalozi wasimamie utekelezwaji wa hilo.




