Jeshi la Polisi limetangaza kuwasaka vigogo nane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wengine wawili kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uporaji, uharibifu wa mali na vurugu siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Kati ya vigogo hao wanaosakwa, yumo Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Mjumbe wa Kamati Kuu (Godbless Lema), Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani (Boniface Jacob) na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Deogratius Mahinyila).
Wengine ni Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho (Brenda Rupia), Kada wa chama hicho (Hilda Newton), Naibu Katibu Mkuu Bara (Amaan Golugwa), Award Kalonga, Machumu Maximilian ‘Mwanamapinduzi’ pia yumo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Taarifa ya msako huo, imetolewa usiku wa kuamkia leo, Novemba 8, 2025 na Jeshi la Polisi, huku likiwasihi kujisalimisha katika vituo vya polisi vilivyopo karibu yao, mara tu watakapoona taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Oktoba 29 kulitokea matukio ya vurugu, uporaji wa mali, uvunjifu wa amani katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya, pia mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa.
Limesema matukio hayo yalisababisha madhara kwa binadamu, uharibifu wa mali za umma na binafsi na kuleta athari kubwa. Mbali na athari za uhai na maisha ya watu, pia mali za umma zilizochomwa moto ikiwemo ofisi za TRA, Takukuru na Mahakama.
Nyingine ni vituo vya mabasi yaendayo haraka kutoka Kimara Mwisho hadi Magomeni na Morocco, ATM za baadhi ya benki, ofisi za Serikali za mitaa, barabara za lami na zege zilizomwa moto na baadhi ya majengo ya CCM huku magari ya umma na binafsi yakiharibiwa.
“Mali za watu binafsi ziliharibiwa na kuchomwa moto ikiwemo vituo vya mafuta, maduka, magari makubwa na madogo.Walifanya uporaji wa mali na pesa za watu kutoka katika maeneo ya biashara,” imeeleza taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime.
Kwa mujibu wa Misime kupitia taarifa hiyo, pamoja na kwamba waliopanga na kutekeleza uhalifu huo wamekamatwa na kuanza kufikishwa mahakamani, polisi likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako mkali kuwatafuta wengine waliopanga na kuratibu.
“Kufuatia uchunguzi na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, Jeshi la Polisi linawasaka kwa ajili ya kuwakamata Gwajima, Brenda, Mnyika, Lema, Kadutu, Mahinyila, Jacob, Hilda, Golugwa na Kalonga.
“Jeshi la Polisi linawataka kujisalimisha katika vituo vya polisi mara moja watakapoona taarifa hii popote walipo,” ameeleza Misime.
Mapema jana Ijumaa Novemba 7 jumla ya watu 239 akiwemo mfanyabiashara Jennifer Jovin maarufu Niffer walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhaini iliyotokana na vurugu za Oktoba 29, 2025.
Jeshi hilo, limewaonya watu au kikundi cha watu wanaopanga kufanya uhalifu wa namna yeyote na kwamba halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
Katika hatua nyingine, limewatoa hofu Watanzania likiwataka kuendelea na shughuli zao huku likiwaomba kutoa taarifa pale wanapoona dalili yoyote ya uhalifu au uvunjifu wa amani mahali popote ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.




