DAR ES SALAAM – Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), kupitia mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati, umekabidhi rasmi kifaa cha kupima hewa chafu kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kuimarisha ubora na usalama wa teknolojia za kupikia safi nchini.
Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa CookFund unaolenga kuharakisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayoungwa mkono na ajenda ya kitaifa ya kuboresha afya, mazingira na uchumi wa kaya.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, alisema kifaa hicho ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha teknolojia za kupikia zinazozalishwa au kuingizwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa vya ubora na usalama.




“Hii ni hatua kubwa katika kuendeleza harakati za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini. Kifaa hiki kitatumika kupima aina ya gesi au moshi unaotokana na majiko mapya yanayotengenezwa au kuingizwa nchini. Kitasaidia kupunguza gharama za upimaji, kuthibitisha ubora wa vifaa na kuhamasisha wabunifu kuongeza uzalishaji,” alisema dk. mataragio.
Serikali ya Tanzania imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya kaya zinatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kulinda mazingira na afya za wananchi.
Kwa upande wake,Marc Stalsmans, Mkuu wa Rasilimali za Asili kutoka Umoja wa Ulaya (EU), alisema kifaa hicho kitaleta mapinduzi katika sekta ya teknolojia safi za kupikia kwa kusaidia upimaji na usanifishaji wa vifaa kwa gharama nafuu.
“Umoja wa Ulaya unajivunia kushiriki katika jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini Tanzania. Tunatarajia kifaa hiki kitawanufaisha zaidi wabunifu na wazalishaji kwa kupunguza gharama za upimaji, kuchochea ubunifu na kuongeza kasi ya uzalishaji wa majiko bora,” alisema stalsmans.




Kwa mujibu wa taarifa ya UNCDF, Mradi wa CookFund umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya nishati safi nchini. Hadi sasa, mradi huo umetoa ruzuku kwa biashara 78, kusaidia shule 41 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, kunufaisha watu zaidi ya milioni 1.7 na kuunda ajira zaidi ya 11,600.
Shigeki Komatsubara, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa UNCDF Tanzania, alibainisha kuwa kifaa hicho kitatoa takwimu muhimu zitakazosaidia kutathmini athari za majiko yasiyokidhi viwango, hatua itakayosaidia kulinda afya za watumiaji na mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, alisema kupatikana kwa kifaa hicho nchini ni hatua muhimu itakayopunguza gharama za upimaji na kuongeza ufanisi katika usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi.
“Kupatikana kwa kifaa hiki nchini ni hatua muhimu katika kupunguza gharama na kusogeza mbele juhudi za usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi. Tunaomba msaada zaidi ili huduma hizi zifikiwe na wananchi katika mikoa mingine kama Dodoma, Mbeya na Mwanza,” alisema Dkt. Katunzi.
Kupatikana kwa kifaa hiki kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa TBS katika kutoa ithibati na udhibiti wa viwango vya teknolojia safi za kupikia, hivyo kuimarisha ubora wa bidhaa zinazowafikia watanzania na kuchochea mapinduzi ya nishati safi nchini.





