Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Janus Mfaume, anatuhumiwa na mwanachama wa chama hicho, Egon Haule, kumdhalilisha na kumtishia maisha baada ya kumzuia kufika katika ofisi za chama hicho.
Haule anadai kuwa tukio hilo lilitokea Julai 17 mwaka huu katika ofisi za CCM Wilaya ya Kilosa, baada ya kufika kuitikia wito wa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi aliyemhitaji kwa ajili ya kumpa majukumu.
Akizungumza kwa masikitiko, Haule alisema tukio hilo ni mara ya tatu kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na vitisho kutoka kwa Mfaume, akidai kuwa amekuwa akizuiwa kufika katika ofisi za chama bila kupewa sababu za msingi.
Alisema hana mgogoro wowote binafsi na Katibu huyo, lakini amekuwa akishangazwa na kauli anazodai zimekuwa zikielekezwa kwake mara kwa mara.
“Mimi ni mwanachama halali ambaye nimekuwa nikijitolea majukumu mbalimbali ya chama kupitia UVCCM Wilaya, lakini nimekuwa nikikumbana na manyanyaso na kufukuzwa kila ninapofika ofisini,” alisema Haule.
Haule alisema kabla ya tukio hilo alikuwa amemtumia ujumbe Mfaume akimuomba wakutane ili aelezwe sababu za kuzuiwa kufika ofisini, lakini hakupata majibu.
Katika ujumbe aliowasilisha kwenye kundi la mawasiliano la chama hicho, Haule alisema anaiomba mamlaka husika kuingilia kati suala hilo kwa kuzingatia haki, taratibu za chama na misingi ya uongozi.
Alisema ana kumbukumbu za mawasiliano ya sauti yanayohusiana na tukio hilo, ambazo yuko tayari kuziwasilisha kwa mamlaka husika endapo zitahitajika.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilosa, Janus Mfaume, alikiri kumzuia Haule kufika katika ofisi hizo, akisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kile alichodai kuwa ni mwenendo usioridhisha wa mwanachama huyo.
Mfaume alidai kuwa Haule amekuwa akijihusisha na vitendo vinavyokichafua chama na kwamba taarifa zake zipo katika vyombo vya dola.
“Huyu kijana amekuwa akifanya mambo mbalimbali yanayokichafua chama, ikiwemo kujifanya mmoja wa maofisa wa CCM Wilaya kwa maslahi yake binafsi,” alisema Mfaume.
Alisema akiwa kiongozi wa chama hicho wilayani ana wajibu wa kulinda maslahi ya ofisi na mali za chama, hivyo aliamua kumzuia Haule kufika ofisini kwa sababu, kwa mujibu wake, hana jukumu rasmi ndani ya ofisi hizo.
Kuhusu tuhuma za vitisho vya maisha, Mfaume alizikanusha na kusema kama mlalamikaji ana ushahidi wa kutosha anaweza kufuata taratibu za kisheria kwa kufikisha suala hilo katika vyombo husika.




