HomeBiasharaWaziri wa Fedha aipongeza TPA kwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Tanga 

Waziri wa Fedha aipongeza TPA kwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Tanga 

Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar ameipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Tanga kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya bandari hiyo, hatua ambayo imeiwezesha kupokea meli kubwa za mizigo kutoka mataifa mbalimbali duniani na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Balozi Omar amesema hayo alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Bandari hiyo, ambapo alieleza kuridhika na mafanikio yaliyopatikana baada ya Serikali kuboresha kina cha Bandari na kujenga gati mpya yenye urefu wa mita 456, ambalo sasa linaruhusu meli kubwa za mizigo kuingia na kutia nanga.

Amesema mafanikio hayo yameifanya Bandari ya Tanga kupokea kwa mara ya kwanza meli kubwa za mizigo zilizotoka moja kwa moja nchini Marekani na China, mataifa yenye uchumi wa kwanza na wa pili kwa ukubwa duniani, jambo linalodhihirisha kuongezeka kwa ushindani na uwezo wa Bandari hiyo katika kuhudumia biashara ya kimataifa.



“Awali kina cha Bandari hakikuruhusu meli kubwa kuingia moja kwa moja. leo hii, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, Bandari ya Tanga imeanza kupokea meli kubwa kutoka Marekani na China moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa yanayostahili pongezi,” amesema Balozi Omar.

Aidha, ameeleza kuwa mipango ya Serikali ya kuongeza urefu wa gati kutoka mita 456 hadi mita 900 kwa ajili ya kuhudumia makasha (containers) itaongeza zaidi uwezo wa Bandari ya Tanga na kuiwezesha kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Balozi Omar amesema ongezeko la uwezo wa Bandari hiyo linafungua fursa mpya za uwekezaji kwa sekta binafsi, hususan katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mizigo na utoaji wa huduma za vifaa vya usafirishaji nje ya eneo la Bandari, huku akiwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Tanga kuzitumia ipasavyo fursa hizo.

“Pamoja na huduma za sasa za usafiri wa abiria kati ya Tanga na Pemba, Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha Bandari ya Tanga kupokea meli za kitalii (cruise ships), hatua itakayochochea ukuaji wa sekta ya utalii na shughuli nyingine za kiuchumi katika mkoa huu” amesema Balozi Omar



Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Tanga,Salehe Mbega, amesema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika upanuzi wa gati na kuongeza kina cha Bandari umebadili kwa kiasi kikubwa uwezo wake ambapo sasa inapokea meli kubwa zinazowasili moja kwa moja (direct call) kutoka mataifa mbalimbali badala ya kutegemea meli ndogo (feeder vessels) kama ilivyokuwa awali. 

Mbega amesema maboresho hayo pia yameongeza kasi ya kuhudumia mizigo kwa kupunguza muda wa kuhudumia meli kutoka wastani wa siku nane hadi kumi hadi kufikia siku tatu hadi tano, sambamba na kuondoa gharama zilizokuwa zikitokana na uhamishaji wa mizigo kutoka baharini kwenda gatini. 

Aidha, amesema idadi ya meli zinazohudumiwa imeongezeka kutoka wastani wa meli 100 kwa mwaka kabla ya maboresho hadi meli 616 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026, huku kiwango cha shehena kikiongezeka kutoka takribani tani 500,000 hadi kufikia tani milioni 2.17 kwa mwaka. 

Ameeleza kuwa Bandari ya Tanga sasa inahudumia pia mizigo mikubwa ya miradi ya kimkakati ya Serikali ikiwemo miradi ya umeme, gesi na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

“Maboresho yaliyofanywa yameongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa Bandari ya Tanga, kiasi kwamba ndani ya miaka miwili hadi mitatu tu tumeanza kushuhudia ongezeko kubwa la meli na shehena kuliko tulivyotarajia. 

Hali hiyo imeifanya Bandari kuanza kufikia ukomo wa uwezo wake, ndiyo maana tunaendelea na mpango wa awamu inayofuata wa upanuzi wa gati tatu na kuongeza maeneo ya kuhifadhi mizigo kwa kushirikiana pia na sekta binafsi kupitia bandari kavu (dry ports),” alisema Bw. Salehe Mbega.

Katika Ziara hiyo Balozi Omar ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini, Dadi Kolimba, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mcha Hassan Mcha, na Makamishna na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zake.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments