HomeMichezoTracy kuiwakilisha Tanzania Miss Supranational Poland

Tracy kuiwakilisha Tanzania Miss Supranational Poland

Tanzania imeandika historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kimataifa ya Miss Supranational 2026, hatua inayotarajiwa kuifungulia nchi fursa zaidi za kuitangaza kimataifa kupitia utalii, utamaduni na sekta ya ubunifu.

Mrembo Tracy Nabukeera ndiye atakayeipeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo yatakayofanyika nchini Poland mwishoni mwa mwezi huu, huku Serikali na wadau wa sekta ya sanaa wakieleza matumaini makubwa kuwa ushiriki huo utaongeza hadhi ya nchi katika majukwaa ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga Tracy iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Afisa Sanaa Mwandamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, aliyemwakilisha Katibu Mtendaji wa baraza hilo, alisema Serikali inaunga mkono ushiriki wa mrembo huyo kwa kuwa anaiwakilisha Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Alisema Tracy amekabidhiwa bendera ya Taifa kama ishara ya imani ambayo Serikali imeweka kwake, akieleza kuwa ana kila sababu ya kufanya vizuri na kuitangaza Tanzania mbele ya mataifa mbalimbali.

Ndaga aliwataka Watanzania kumuunga mkono Tracy kwa kumpigia kura wakati wote wa mashindano ili kuongeza nafasi ya nchi kufanya vizuri na kuibuka na ushindi.

“Natoa wito kwa Watanzania wote kumuombea na kumpigia kura kwa wingi Tracy ili aipeperushe vyema bendera ya Tanzania na kuongeza nafasi ya kushinda taji hilo,” alisema.

Alisema sekta ya sanaa imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa kwa kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi.

“Sanaa ni ajira na ni uchumi. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya ubunifu ili kuhakikisha vipaji vya Watanzania vinapata fursa ya kushindana na kuonekana katika majukwaa ya kimataifa,” alisema.

Kwa upande wake, mratibu wa mashindano hayo nchini, Millen Magesa, alisema ushiriki wa Tanzania katika Miss Supranational ni hatua ya kihistoria inayofungua ukurasa mpya wa kuitangaza nchi kupitia utalii, utamaduni na uwezo wa wanawake wa Kitanzania.

Alisema Tracy anakwenda Poland akiwa balozi wa Tanzania na amebeba matumaini ya Watanzania wengi wanaotaka kuona nchi ikifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Aidha, alisema hatua hiyo itakuwa chachu kwa wasichana na wanawake wengi nchini kuamini ndoto zao na kuthubutu kushiriki katika majukwaa ya kimataifa, huku ikionyesha kuwa vipaji vya Watanzania vinaweza kushindana na kufanya vizuri duniani.

Tracy ameondoka kuelekea Poland kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo, huku Serikali na waandaaji wakitoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea, kumpigia kura na kumpa sapoti katika safari yake ya kuiwakilisha Tanzania kimataifa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments