Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema mafanikio yanayoendelea kupatikana katika ukamataji wa dawa za kulevya na wahalifu wake nchini yametokana kwa kiasi kikubwa na mchango wa vyombo vya habari.
Lyimo ameyasema hayo leo wakati wa kikao kazi cha kutathmini mchango wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, akibainisha kuwa taarifa na ripoti za wanahabari zimekuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha kazi za DCEA.
Amesema pongezi zinazotolewa kwa Tanzania kutoka mataifa mbalimbali zinatokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari kupitia kalamu zao, kwa kuripoti kwa ufasaha na ujasiri shughuli na mafanikio ya DCEA katika kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, Lyimo ameeleza kuwa dawa za kulevya ni chanzo kikuu cha watu kujiingiza katika vitendo vya ugaidi, akisisitiza kuwa mtu anayejihusisha na ugaidi mara nyingi hutumia dawa hizo. Ameongeza kuwa fedha zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya pia hutumika kufadhili matukio ya ugaidi, hali inayozifanya dawa hizo kuwa tishio kubwa kwa usalama wa taifa.




