Friday, February 20, 2026
spot_img
HomeBiasharaWenye Bandari Kavu matatani ukwepaji kodi

Wenye Bandari Kavu matatani ukwepaji kodi

Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema kuna wamiliki wa Bandari Kavu (ICDs) ambao wamekuwa wakikwepa kodi kwa kutumia njia mbalimbali na ameahidi kuwachukulia hatua kali kukomesha hali hiyo.

Kamishna Mwenda aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mamlaka hiyo na wanachama wa chama cha wamiliki wa Bandari Kavu nchini lengo ikiwa ni kusikiliza kero zao.

Alisema TRA itakuwa inakaa na wanachama hao kila baada ya miezi mitatu kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi na pia mamlaka hiyo itakuwa inatumia fursa hiyo kuwaeleza kuhusu baadhi yao wanaofanya ujanja huo wa kukwepa kodi.

“Tutakutana nanyinyi ili mtueleze ya kwenu nasisi tuwaeleze ya kwetu, tunajua kinachoendelea huko, kuna baadhi yenu wanazitumia ICDs kukwepa kodi, na tukiwaambia mnasema ni maofisa wenu walioko huko,sisi tunajua na nawaambia tutachukua hatua kukomesha hali hiyo,” alisema Kamishna Mwenda

“Kwenye vikao vyetu hivyo tutawaeleza mlipoteleza na sisi mtuambie tulipokosea, mfano kwenu nyingi shida naiona kwenye utoaji wa maamuzi kwasababu wengi mnakuwa hampo kwenye maeneo yenu ya kazi kwa hiyo mhakikishe kama haupo umekabidhi majukumu kwa mtu mwingine ili aweze kutoa maamuzi,” alisema Kamishna Mwenda


Katika hatua nyingine, Kamishna Mwenda alisema TRA imeweka mkakati kuwawezesha wamiliki wa Bandari Kavu nchini kufanyakazi kwa saa 24 kama mkakati wa kuongeza mapato ya mamlaka hiyo.

Alisema TRA itajitahidi kuongeza idadi ya wafanyakazi kuwezesha hilo kufanyika lakini na wenye bandari kavu nao wanapaswa kuongeza miundombinu ya kuwezesha kufanya kazi saa 24.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi kuhakikisha mizigo inayofika kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kwingineko inatoka kwa haraka kama mkakati wa kuongeza ushindani na bandari za jirani.

“Sisi tunawatazama nyinyi wamiliki wa ICDs kama washirika wetu muhimu sana kwasababu mkikua nasisi tutakua kwa mapato yetu kuongezeka na mkianguka nasisi tutaanguka kwa hiyo tutaendelea kufanya kazi kwa karibu sana kufikia malengo yetu kwa pamoja, tunataka nyinyi mpate na  mamlaka ipate mapato yake stahiki,” alisema


Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Bandari binafsi, Melleck Shangwe alisema amefurahi kusikia kuwa bandari kavu zinachangia mapato yatokanayo na forodha kwa asilimia 52  kila mwaka.


Shangwe aliahidi kuwa kama changamoto zao zitafanyiwa kazi basi wanaweza kuongeza mapato hayo hadi kufikia asilimia 60 katika mwaka ujao wa fedha

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni mkanganyiko wa uwasilishaji wa nyaraka baina ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato TRA kutoka na kila mmoja kuwa na msimamo tofauti kuhusu uwasilishaji wa nyaraka.

“TPA wanasema nyaraka kwanza kabla ya mzigo haujafika wakati TRA wenyewe wanasema mzigo kwanza kabla ya nyaraka kufika sasa hali hii inatuchanganya sisi wenye ICD kwa hiyo tunaomba muwe na msimamo wa pamoja kunusu uwasilishaji wa nyaraka,” alisema

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments