Friday, March 13, 2026
spot_img
HomeBiasharaMgogoro wa Mashariki ya Kati waweza kuongeza bei za mafuta nchini

Mgogoro wa Mashariki ya Kati waweza kuongeza bei za mafuta nchini

Mgogoro wa kijeshi unaoendelea kati ya Marekani/Israel na Iran umeanza kuleta taharuki katika soko la mafuta duniani, hali inayoweza kuathiri upatikanaji na bei za mafuta nchini Tanzania iwapo vita hivyo vitaendelea kwa muda mrefu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoagiza mafuta kutoka nje, baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta kufungwa miaka ya 1990. Kwa sasa, mafuta yote yanayoingia nchini huagizwa kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) unaoratibiwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA). Kupitia mfumo huo, PBPA hutoa zabuni kila mwezi kwa kampuni zilizokidhi vigezo, na kampuni yenye gharama ndogo ya uagizaji hupata zabuni ya kuleta mafuta nchini.

Katika kipindi cha miezi sita hadi Machi 2026, Tanzania imeagiza mafuta kutoka nchi mbalimbali ikiwemo India kwa asilimia 40, Falme za Kiarabu (UAE) asilimia 37, Saudi Arabia asilimia 8, Oman asilimia 8, Kuwait asilimia 4 na Bahrain asilimia 2.

Hata hivyo, utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi, hasa kutoka Mashariki ya Kati, unaifanya Tanzania kuwa katika hatari ya kuathiriwa na migogoro ya kisiasa inayotokea katika eneo hilo.

Taharuki katika Soko la Mafuta Duniani

Tarehe 28 Februari 2026, mashambulizi kati ya Marekani/Israel na Iran yalizua taharuki katika soko la mafuta duniani. Mashariki ya Kati huzalisha zaidi ya asilimia 30 ya mafuta ghafi yanayouzwa duniani, huku Iran ikichangia takribani asilimia 4.5 ya uzalishaji huo.

Iwapo mafuta kutoka Iran yatapungua katika soko la dunia, nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran, hususan China, zitalazimika kutafuta vyanzo vingine vya mafuta na hivyo kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.

Aidha, hofu ya mashambulizi katika miundombinu muhimu ya mafuta katika nchi jirani kama Saudi Arabia, Bahrain na Falme za Kiarabu imeongeza hatari ya kuvurugika kwa uzalishaji na usambazaji wa mafuta duniani.

Njia nyingine muhimu ya usafirishaji wa mafuta ni Lango la Hormuz ambalo hupitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yote yanayosambazwa duniani. Endapo njia hiyo itafungwa au kusumbuliwa kutokana na vita, usafirishaji wa mafuta unaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Tayari baadhi ya kampuni za usafirishaji na bima zimeanza kupunguza shughuli zao katika eneo hilo kutokana na hatari za vita.

Katika siku chache tangu kuanza kwa mgogoro huo, bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia imeanza kupanda. Bei ya mafuta aina ya Brent iliongezeka kutoka takribani dola 72 kwa pipa hadi zaidi ya dola 80 kwa pipa kufikia tarehe 3 Machi 2026. Wataalamu wanakadiria kuwa iwapo vita vitaendelea kwa muda mrefu, bei ya mafuta inaweza kufikia zaidi ya dola 100 kwa pipa.

Athari Zinazoweza Kujitokeza Tanzania

Kutokana na utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi na kukosekana kwa hifadhi ya kimkakati ya mafuta, mgogoro huo unaweza kuwa na athari kadhaa nchini.

Moja ya athari zinazoweza kujitokeza ni ongezeko la bei za mafuta nchini kutokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia. Migogoro ya kisiasa huathiri haraka masoko ya mafuta na kusababisha mabadiliko ya bei kimataifa.

Aidha, gharama za uagizaji wa mafuta zinaweza kuongezeka kutokana na hatari za usalama katika njia za usafirishaji, kuongezeka kwa gharama za bima na uwezekano wa kutumia njia mbadala za usafirishaji ambazo huchukua muda mrefu zaidi.

Kupanda kwa bei za mafuta pia kunaweza kuongeza mahitaji ya fedha za kigeni, hasa dola za Marekani, ambazo hutumika katika uagizaji wa mafuta. Hali hii inaweza kuongeza shinikizo katika akiba ya fedha za kigeni na kuathiri uwezo wa nchi kuagiza mafuta kwa gharama nafuu.

Vilevile, ongezeko la bei za mafuta linaweza kusababisha mfumuko wa bei wa bidhaa na huduma nyingine kutokana na gharama kubwa za usafirishaji na uzalishaji.

Changamoto nyingine inayoweza kujitokeza ni ongezeko la gharama za meli kusubiri bandarini (demurrage) iwapo kutakuwa na ucheleweshaji wa safari za meli na msongamano wa meli bandarini.

Hatua za Kupunguza Athari

Wataalamu wanaeleza kuwa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, kuna umuhimu wa kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na muda mrefu.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuhamasisha matumizi ya gesi asilia iliyokandamizwa (CNG) katika magari ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli, hususan katika usafiri wa mijini.

Aidha, inapendekezwa kuongeza akiba ya mafuta ya dharura kutoka kiwango cha sasa cha siku 15 hadi angalau siku 20 ili kuimarisha usalama wa upatikanaji wa mafuta nchini.

Hatua nyingine muhimu ni kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve – SPR) kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015. Hifadhi hiyo itasaidia kuhakikisha nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta wakati wa dharura au changamoto katika soko la dunia.

Pia kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mwenendo wa soko la mafuta duniani, ili kusaidia jamii kuelewa sababu za mabadiliko ya bei za mafuta nchini.

Hitimisho

Kutokana na utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi, hasa kutoka Mashariki ya Kati, Tanzania inaweza kuathiriwa na mgogoro unaoendelea kati ya Marekani/Israel na Iran.

Hata hivyo, utekelezaji wa mikakati madhubuti kama kuimarisha akiba ya mafuta, kuanzisha hifadhi ya taifa ya mafuta na kupanua matumizi ya nishati mbadala unaweza kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya soko la mafuta duniani kwa uchumi wa nchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments