Watumishi wa idara ya Kamati za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameridhishwa na huduma zinatolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa watumishi wa Umma (PSSSF) na wameshauri PSSSF izidishe ubunifu ili kurahisisha huduma kwa Wanachama wake.
Kauli hiyo imetolewa Julai 31, 2026 mjini Morogoro katika semina iliyoendeshwa na PSSSF maalum kwa Watumishi wa Bunge ambayo iliwashirikisha Makatibu wote wa kamati za Bunge. Semina ilikuwa ya kuwajengea uwelewa wa Kinga ya Jamii, hususani PSSSF.
“Hongereni sana matumizi ya mtandao hivi sasa mambo mmeyarahisisha sana, kwani kila kitu kinaanzwa na kumalizwa kwenye simu au kifaa kingine chochote cha kidijitali” alisema Angelina Sanga.


Aidha, wajumbe wa semina hiyo walishauri sera ya Kinga ya Jamii ipitiwe ili iweze kwenda na wakati.
Katika semina hiyo Mtumishi Mstasaafu wa Bunge Gerald Magili alithibitisha kuwa PSSSF ‘inalipa jana’ kwa kusema, “Nilitoa taarifa ya kuomba kibali cha kustaafu kwa mwajiri miezi sita kabla ya kusataafu, tarehe yangu ya kustaafu ilikuwa ni Juni 25, 2026, siku hiyo hiyo nilipokea mafao yangu ya kustaafu, hakika PSSSF mpo vizuri”.
Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSSSF, Hajji Moshi alishukuru ofisi ya Bunge kwa kutoa nafasi ya kufanyika semina hiyo na kusema kuwa Mfuko uko tayari wakati wowote kutoa elimu ya Kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Bunge na Wanachama wengine.

“Kwa niaba ya Menejimenti ya PSSSF, tunashukuru kupokea maoni kutoka kwenu, yote tumeyachukua na tutayafanyia kazi na yale ya Kisera tutayafikisha kwa Mamlaka husika, asanteni sana” alisema Hajji Moshi.
Kwa upande wake, Michael Chikokoto, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Kamatii za Bunge, alisema, “Tunawashukuru PSSSF kwa kuitikia wito wetu, naamini tumejifunza mengi na tatakuwa mabalozi wenu kwa watumishi wengine wa Bunge.





