Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) umezalisha ajira 31,875 katika mwaka wa fedha 2025/26 kupitia shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani wa mazao na bidhaa.
Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Asangye Bangu katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Idara ya Habari – MAELEZO wa kutangaza utekelezaji wa shughuli za kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27.
Bangu, amesema ajira hizo zimetokana na shughuli za ukusanyaji wa mazao na bidhaa, uhifadhi ghalani, upimaji wa ubora, usafirishaji, upakiaji na upakuaji pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na biashara kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Aidha, amesema mchango wa WRRB katika kuongeza mapato ya Serikali umeendelea kuimarika, ambapo fedha zilizorejeshwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali zimeongezeka kutoka Sh. milioni 22 mwaka wa fedha 2023/24 hadi kufikia Sh. milioni 140 mwaka 2025/26.
Akizungumzia kuhusu ukaguzi wa bidhaa, Bangu amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, magunia 19,041,651 yenye uzito wa zaidi ya kilo bilioni 1.114 yalikaguliwa katika ghala mbalimbali nchini, hatua iliyochangia kuimarisha uaminifu wa mfumo na kulinda maslahi ya wadau wote wa biashara.




