Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yamethibitisha kuwa taarifa zao kuhusu matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyodaiwa kutokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa tarehe 29 Oktoba 2025 nchini Tanzania zilijengwa zaidi kwa maelezo ya upande mmoja bila kuhusisha kikamilifu maelezo kutoka upande wa Serikali na taasisi zake.
Hayo yamebainika katika kikao cha pembezoni mwa Mkutano wa 61 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 12 Machi 2026 mjini Geneva, Uswisi. Kikao hicho kiliandaliwa na mashirika ya Human Rights Watch pamoja na Amnesty International na kuongozwa na Lucy McKernan, Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ulaya, mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali pamoja na wataalamu wa masuala ya haki za binadamu.
Katika kikao hicho ilielezwa kuwa taarifa zilizotolewa kuhusu Tanzania zilijengwa kwa kiasi kikubwa juu ya mahojiano, nyaraka na taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vilivyotoa maelezo ya upande mmoja wa matukio hayo. Aidha, Gina Romero, Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Kukusanyika na Kujumuika, alieleza kuwa katika kuandaa uchambuzi huo walitumia mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa, ikiwemo kufanya mahojiano na kupitia taarifa zilizokuwapo kabla ya kuandaa ripoti hiyo na kuitoa kwa umma.
Katika kikao hicho, mawasilisho yalitolewa na Oryem Nyeko, Mtafiti Mwandamizi wa Shirika la Human Rights Watch kwa Kanda ya Afrika, Tito Magoti, Mwanasheria wa Centre for Strategic Litigation, pamoja na Sikula Oniala, Mtafiti wa Amnesty International. Wawasilishaji hao walielezea masuala mbalimbali waliyoyabaini kuhusu machafuko ya Oktoba 2025 nchini Tanzania, maelezo ambayo yaliendelea kuakisi kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa taarifa za awali zilizotolewa na taasisi hizo.
Hata hivyo, katika mjadala uliofuata ilibainika kuwa taasisi hizo hazikufanya mahojiano ya kina na upande wa walalamikiwa, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi zake, kabla ya kukamilisha taarifa zao. Ilielezwa kuwa pamoja na jitihada za kuwasiliana kwa njia ya barua ili kuomba mahojiano, majibu yalichelewa kupatikana, hali iliyosababisha taarifa hizo kuandaliwa na kutolewa bila kuhusisha kikamilifu maelezo ya upande wa Serikali, ambao ni mhusika muhimu katika suala hilo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya washiriki wa kikao hicho, wakiwemo wawakilishi kutoka Zimbabwe na Ujerumani, walihoji uhalali wa kutegemea taarifa ambazo hazikuzingatia kwa uwiano maelezo ya pande zote zinazohusika. Katika michango yao, walisisitiza umuhimu wa kusubiri taarifa ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kwa mujibu wa hadidu zake za rejea imepewa jukumu la kufanya mahojiano na makundi mbalimbali ya wadau pamoja na kupokea ushahidi, maoni na mapendekezo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupitia mifumo ya mtandaoni.
Washiriki wengine wa kikao hicho walijadili pia mazingira yaliyokuwapo wakati wa matukio hayo, ikiwemo hatari ya uharibifu wa mali na uwezekano wa vifo vya watu. Katika mjadala huo ilielezwa kuwa katika mazingira kama hayo Serikali ilikuwa na wajibu wa kutumia njia halali za kisheria kudhibiti hali hiyo na kulinda usalama wa wananchi pamoja na mali zao. Wakati huohuo, ilisisitizwa kuwa uwajibikaji unapaswa kuzingatia pande zote, ikiwemo watu wa ndani na nje ya Tanzania waliotumia lugha za uchochezi kabla na baada ya uchaguzi kwa namna iliyoweza kuchangia kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Aidha, mjumbe kutoka Ujerumani alitoa angalizo kuhusu umuhimu wa kufuatiliwa kwa makini kwa mienendo ya uchochezi katika nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2027, ili kuzuia kujirudia kwa matukio yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa eneo hilo.
Kwa ujumla, mjadala uliofanyika katika kikao hicho umeonesha umuhimu wa taarifa za uchunguzi kujengwa juu ya usikilizwaji wa pande zote zinazohusika ili kuhakikisha uwiano, uhalisia na uaminifu wa taarifa zinazowasilishwa kwa umma wa kimataifa. Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa uchunguzi unaozingatia ushahidi, uwiano wa taarifa na taratibu za haki ili kuimarisha amani, utulivu na utawala wa sheria.




