Uzoefu wa Tanzania katika kuunganisha uhifadhi wa maliasili na maendeleo ya sekta ya utalii umevutia wataalamu kutoka nchini Zambia, waliowasili nchini kwa ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu.
Ujumbe huo umetembelea Tanzania Machi 16,2026 kwa lengo la kujifunza namna nchi inavyotekeleza mikakati ya uhifadhi wa rasilimali za asili sambamba na kutangaza vivutio vyake vya utalii katika masoko ya kimataifa.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ujumbe huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Ephraim Mafuru amesema nchi imeendelea kuwa ya mfano barani Afrika kuunganisha juhudi za uhifadhi na maendeleo ya utalii, hatua inayochangia kukuza uchumi wa taifa.


Amesema mfumo wa usimamizi wa hifadhi, uendelezaji wa vivutio vya utalii pamoja na mikakati ya masoko ya kimataifa umeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazoongoza kwa kuvutia watalii duniani.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Baraza la Mawaziri ( FED) kutoka nchini Zambia Siazongo Siakalenge, pamoja na wataalam kutoka sekta ya utalii, uhifadhi wa wanyamapori wameongoza ujumbe huo.


Wajumbe wa Zambia wameeleza kuvutiwa na juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kulinda rasilimali za asili huku ikiendeleza utalii kama kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
“Kama sehemu ya ziara yao ya mafunzo, ujumbe huo pia umetembelea Hifadhi ya Serengeti, kushuhudia uhamaji mkubwa wa nyumbu tukio la kipekee duniani linalovutia maelfu ya watalii kutoka mataifa mbalimbali kila mwaka,” amesema Siakalenge.





