Na WMJJWM – New York, Marekani
Tanzania imeendelea kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana kama sehemu ya juhudi za kufanikisha usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Hayo yameelezwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Barke Sehel, alipokuwa akifungua mjadala maalum ulioandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, pembezoni mwa mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani.
Amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia pamoja na kujadili changamoto zinazowakwamisha wanawake na wasichana kufurahia haki zao kikamilifu.
Jaji Sehel amesisitiza kuwa huduma za msaada wa kisheria zina mchango mkubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia, akieleza kuwa upatikanaji wa haki haupaswi kubaki kuwa nadharia bali utekelezwe kwa vitendo kupitia mifumo imara ya msaada wa kisheria.
“Bila msaada madhubuti wa kisheria, ulinzi dhidi ya ukatili, ubaguzi na kutengwa hubaki kuwa ndoto kwa wanawake na wasichana wengi,” amesema.




Kwa mujibu wake, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuimarisha mifumo ya haki jumuishi kwa kuongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sambamba na kuzingatia makubaliano ya kimataifa kama Azimio la Beijing na Itifaki ya Maputo.
Amefafanua kuwa hatua muhimu iliyochukuliwa ni kutungwa kwa sheria za msaada wa kisheria kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambazo zimepanua wigo wa huduma hizo kutoka masuala ya jinai pekee hadi kujumuisha pia masuala ya kiraia na watoto.
Hatua hiyo imewasaidia wanawake na wasichana kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo migogoro ya urithi, haki za ardhi, migogoro ya kifamilia pamoja na ukatili wa kijinsia.
Aidha, amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka kipaumbele katika upatikanaji wa haki kwa wanawake kama msingi wa maendeleo jumuishi, ikitambua mchango wao katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.





Akizungumzia juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia, Jaji Sehel amesema msaada wa kisheria unawawezesha waathirika kuripoti matukio, kufuatilia haki zao na kupata ulinzi unaostahili.
Ameongeza kuwa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria iliyoanzishwa chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan, imesaidia kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, hasa wanawake na wasichana wa maeneo ya vijijini.
Jaji Sehel ametoa wito kwa nchi wanachama na wadau kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki zao kikamilifu.
Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa kuhakikisha hakuna mwanamke au msichana anayebaki nyuma katika mapambano ya kupata haki na kutokomeza ukatili wa kijinsia.





