Wednesday, March 18, 2026
spot_img
HomeHabariRC Chalamila ahamasisha upendo bila ubaguzi

RC Chalamila ahamasisha upendo bila ubaguzi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi kuendelea kudumisha mshikamano na kuishi kwa upendo bila kujali tofauti za kidini, akisisitiza kuwa umoja ni msingi wa amani na maendeleo ya taifa.

Amesema ni muhimu kwa jamii kuendeleza utamaduni wa kupendana, kuthaminiana na kusaidiana bila kuangalia hadhi au muonekano wa mtu, akibainisha kuwa mafundisho hayo yanahimizwa na dini mbalimbali.

Chalamila ametoa wito huo wakati wa hafla ya Iftar iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliyowakutanisha watu wenye matatizo ya kuona pamoja na watoto kutoka vituo vya kulea yatima. Amesisitiza kuwa vipindi kama mwezi mtukufu wa Ramadhani vinapaswa kuwa chachu ya kuonyesha upendo kwa makundi maalum yenye uhitaji.

Ameongeza kuwa mshikamano, upendo na ushirikiano vinapaswa kuendelezwa wakati wote, si katika kipindi cha Ramadhani pekee, ili kuimarisha amani na utulivu wa nchi.

Aidha, ameeleza kuwa hafla za Iftar zina mchango mkubwa katika kuwaleta pamoja watu wa dini tofauti, hali inayojenga uelewano na kuimarisha mahusiano ya kijamii.

“Ni muhimu kuendeleza utamaduni wa kupendana na kusaidiana bila kujali dini zetu, kwani sisi sote ni Watanzania,” amesisitiza Chalamila.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa dini, wadau mbalimbali pamoja na wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuwajali zaidi watu wenye uhitaji katika jamii.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments