Wednesday, March 25, 2026
spot_img
HomeHabariTanzania yakabidhi msaada wa mahindi kwa Msumbiji

Tanzania yakabidhi msaada wa mahindi kwa Msumbiji

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi msaada wa tani 500 za mahindi kwa Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kufuatia mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo kutokana na mvua kubwa zilizonyesha.

Msaada huo umekabidhiwa Machi 24, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Shehena hiyo ya mahindi iliwasili jijini Maputo na ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Tanzania na kupokelewa na Ujumbe wa Serikali ya Msumbiji uliongozwa na Waziri wa Mipango na Maendeleo, Mhe. Salim Cripton Valá,

Akikabidhi msaada huo, Mhe. Kombo alielezea uhusiano wa karibu na wakindugu uliopo baina ya Tanzania na Msumbiji ulioasisiwa tokea enzi za waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Juliaus Kambarage Nyerere na Hayati Edward Mondlane. Waziri Kombo alisema kufuatia udugu huo, Rais Dkt. Samia amemtuma kufikisha msaada huo ili uweze kuwapunguzia adha waathirika wa mafuriko hayo.

“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Rais Samia anatoa salamu za pole kwa Rais wa Msumbiji, Mhe. Daniel Chapo na watu wa Msumbiji kwa ujumla kutokana na madhila yaliyosababishwa na mafuriko haya na ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kundelea kutoa msaada kwa Msumbiji katika nyakati zote”, Waziri Kombo alisema.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kombo alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Maria Belvinda Levy kuhusu kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, hususani kwenye masuala ya kiuchumi.

Serikali ya Msumbiji imetoa shukrani za dhati kwa kupokea msaada huo kutoka kwa ndugu zao Watanzania ambao unabainisha taswira ya ukaribu na ushirikiano wa kweli uliopo baina ya nchi mbili hizi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments