DODOMA — Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Mkapa Foundation zimeandaa kambi ya huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka sita tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.
Akizungumza Mei 29, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema mwaka huu taasisi hizo zimeamua kuadhimisha kumbukumbu za Hayati Mkapa kwa kuwafikishia wananchi huduma za afya badala ya kufanya mikutano na makongamano kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Amesema huduma hizo zitatolewa kuanzia Juni 1 hadi 5, 2026 katika Wilaya ya Masasi, ambako Hayati Mkapa alizaliwa, zikilenga kuwahudumia wananchi kwa matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.

Profesa Makubi amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa imebeba jina la kiongozi huyo kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya alipokuwa mtumishi wa umma na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi, madaktari bingwa wabobezi watatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na shinikizo la damu, saratani, kisukari, magonjwa ya watoto, figo, sikoseli pamoja na huduma za upasuaji na upandikizaji wa uloto.
Ameongeza kuwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, BMH itatumia magari maalumu yenye teknolojia za kisasa yaliyo na vyumba vya upasuaji na vifaa tiba mbalimbali, yatakayotoa huduma hata katika maeneo ya vijijini.
Magari hayo yalizinduliwa mwaka 2025 kupitia ushirikiano kati ya BMH na Shirika la SOTAC la Uholanzi, na tayari yamefanikiwa kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Burundi, Singida na Zanzibar.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya diplomasia yaliyowezesha ushirikiano huu. Huduma zote zitakazotolewa Masasi zitakuwa bure kwa wananchi,” amesema Profesa Makubi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la SOTAC, Robert Roel Van Den Bos, amesema ushirikiano kati ya shirika hilo na BMH umewezesha huduma za kibingwa kuwafikia wananchi wengi zaidi, huku magari hayo yakibuniwa kwa uwezo wa kufika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.





