HomeBiasharaCRDB yazindua Smart Mifugo inayotumia AI kulinda wafugaji Tanzania

CRDB yazindua Smart Mifugo inayotumia AI kulinda wafugaji Tanzania

DAR ES SALAAM: Kampuni ya CRDB Insurance Company imezindua huduma ya Smart Mifugo, bima ya mifugo inayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI) kuwakinga wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na vifo vya mifugo, magonjwa na athari za ukame.

Huduma hiyo imezinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, kwa ushirikiano kati ya CRDB Insurance Company na Agriculture and Climate Risk Enterprise (ACRE Africa) kupitia jukwaa la DijiBima, ambalo tayari linatumika katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Kenya, Malawi, Sierra Leone, Zimbabwe, Rwanda, Zambia na Nigeria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Agnes amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, hivyo sekta hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Amesema ushirikiano kati ya CRDB Insurance Company na ACRE Africa umeleta teknolojia ya kisasa itakayowawezesha wafugaji kupata huduma za bima kwa njia ya kidijitali kwa urahisi, usalama na uwazi zaidi.

“Matumizi ya akili mnemba katika kutambua alama ya pua ya mnyama ni hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya mifugo. Ubunifu huu utaongeza uaminifu, kupunguza udanganyifu na kuboresha utoaji wa huduma za bima,” amesema Agnes.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amesema huduma hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazotokana na mbinu za jadi za kutambua mifugo, ikiwemo kupiga chapa ng’ombe, ambayo hupunguza ubora wa ngozi.

“Tumekuja na teknolojia ya akili mnemba inayotambua mnyama kupitia alama ya pua yake. Hii itaondoa madhara ya mbinu za zamani na kurahisisha utambuzi wa mifugo kwa usalama zaidi,” amesema Dk. Nsekela.

Ameongeza kuwa baada ya uzinduzi nchini Tanzania, huduma hiyo itapanuliwa katika nchi zote ambazo Benki ya CRDB inafanya shughuli zake, ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambazo pia zina idadi kubwa ya mifugo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava, amewahimiza wafugaji kote nchini kutumia huduma hiyo ili kujikinga dhidi ya majanga yanayoweza kusababisha hasara kubwa.

“Huduma hii sasa inapatikana katika matawi yote ya CRDB Insurance nchini. Tunawaalika wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo kutembelea matawi yetu yaliyo karibu nao ili kupata huduma hii na kulinda uwekezaji wao,” amesema Mnzava.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments