DAR ES SALAAM: Kampuni ya mawasiliano ya Halotel Tanzania imezindua rasmi ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama SabaSaba, kwa kuwasilisha huduma na teknolojia mbalimbali za kidijitali zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ikiwa na kaulimbiu “Teknolojia kutoka Moyoni,” Halotel imesema inaendelea kuimarisha dhamira yake ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini kupitia huduma bunifu za mawasiliano, intaneti na huduma za kifedha.
Wageni wanaotembelea banda la Halotel watapata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali ikiwemo mtandao wa 5G, huduma ya intaneti ya kasi ya juu ya HaloFibre, suluhisho za kidijitali kwa biashara pamoja na huduma za kifedha za HaloPesa.
Kupitia HaloPesa, wateja wanaendelea kunufaika na huduma salama na rahisi za kutuma na kupokea fedha, kuweka na kutoa fedha pamoja na kufanya malipo kidijitali, hatua inayochangia kuimarisha ujumuishaji wa kifedha nchini.
Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya HaloPesa, kampuni hiyo imeandaa ofa maalumu, zawadi na shughuli mbalimbali za kuwashirikisha wateja ili kuboresha uzoefu wao katika kipindi chote cha maonesho.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushiriki wa Halotel katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Halotel Tanzania, Abdallah Salum, alisema SabaSaba ni jukwaa muhimu linaloiwezesha kampuni kukutana ana kwa ana na wateja wake, kusikiliza mahitaji yao na kuonesha ubunifu unaoboresha maisha kupitia teknolojia.
“SabaSaba inatupatia jukwaa muhimu la kukutana ana kwa ana na wateja wetu, kusikiliza mahitaji yao na kuonesha ubunifu unaoendelea kuboresha maisha yao kupitia teknolojia,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania, Tran Thi Thuy Dung, alisema kampuni itaendelea kuwekeza katika ubunifu unaolenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini.

Alisema kupitia maonesho hayo, wageni watapata nafasi ya kujionea kwa vitendo huduma zinazotolewa na Halotel pamoja na manufaa yake katika maisha ya kila siku.
Naye Meneja wa Masoko wa HaloPesa, Aidat Lwiza, alisema maadhimisho ya miaka 10 ya huduma hiyo yameambatana na ofa na zawadi maalumu zitakazowawezesha wateja wengi zaidi kufurahia huduma salama, rahisi na zenye uhakika za kifedha kidijitali.
Halotel imewaalika wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya teknolojia kutembelea banda lake katika Maonesho ya SabaSaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam ili kujionea huduma zake za kidijitali na kunufaika na ofa mbalimbali zitakazotolewa kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.





