Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na wadau kupitia ubunifu mpya uliooneshwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka 2026.
Kwa mujibu wa Afisa Mifumo wa PSSSF, Bw. Gerald Minza, mfuko huo umeanzisha mfumo wa kisasa wa huduma kupitia “meza janja” (Smart Table), ambayo ni kompyuta iliyounganishwa ndani ya meza maalum inayomwezesha mteja kujihudumia mwenyewe.
Bw. Minza amesema mteja anapofika kwenye banda la PSSSF hukaribishwa kukaa kwenye kochi mbele ya meza hiyo, ambapo kupitia skrini iliyojengewa ndani, huweza kupata huduma mbalimbali baada ya maelekezo mafupi.




Meya wa Temeke astaajabishwa na teknolojia ya meza janja ya PSSSF
Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo mwanachama anaweza kupata taarifa za michango yake, mafao, kuhuisha taarifa binafsi, kuwasilisha madai, kupata elimu ya hifadhi ya jamii pamoja na taarifa kuhusu uwekezaji wa mfuko huo kwa njia ya kidijitali.
Amesema ubunifu huo ni sehemu ya mkakati wa PSSSF wa kuendelea kuwekeza katika mageuzi ya kidijitali ili kuboresha uzoefu wa wateja, kuongeza ufanisi wa huduma na kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.
“Tunawakaribisha wananchi waje wajionee maajabu ya huduma hizi za kidigitali,” amesema Bw. Minza.
Akizungumzia huduma hiyo, mwanachama wa PSSSF, Bw. Ally Midaka, amesema alishangazwa na ubunifu huo wa meza janja, akisema ni tofauti na kompyuta za kawaida alizowahi kuona.
“Hii kompyuta siyo ya kawaida, tumezoea laptop au desktop, lakini hii ya kama meza sijawahi kuiona,” amesema Midaka baada ya kujihudumia kupitia mfumo huo.





