HomeBiasharaPPAA yawaita wadau ununuzi wa umma Sabasaba kupata elimu 

PPAA yawaita wadau ununuzi wa umma Sabasaba kupata elimu 

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewasihi wadau wa ununuzi wa umma pamoja na wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata elimu kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo, ikiwemo matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria wa PPAA, Bi. Agnes Sayi, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, leo Julai 1, 2026, katika Banda la Wizara ya Fedha kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Bi. Sayi amesema PPAA inatoa elimu kuhusu namna ya kushughulikia rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma, rufaa za wafanyabiashara waliofungiwa kushiriki katika zabuni za umma, pamoja na malalamiko yanayotokana na Afisa Masuuli kushindwa kutoa uamuzi ndani ya muda uliowekwa.

Ameongeza kuwa mamlaka hiyo pia inatoa elimu kuhusu uamuzi wa malalamiko yanayowasilishwa baada ya utekelezaji wa mkataba wa ununuzi kuanza, maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha rufaa, utekelezaji wa amri za Mamlaka ya Rufani, maombi ya kufuta maamuzi yaliyotolewa bila kusikiliza upande mwingine (Ex Parte Decision), pamoja na maombi ya kurejesha rufaa.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yalianza Juni 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026, yakishirikisha taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi kuonesha huduma na bidhaa zao kwa kaulimbiu isemayo, “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments