Dar es Salaam, Julai 8, 202 – Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuwa kutakuwa na kukosekana kwa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga kuanzia Julai 9 hadi Julai 14, 2026, kupisha utekelezaji wa kazi za uvutaji waya (stringing) katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TANESCO, zoezi hilo litahusisha uvutaji wa waya katika njia ya umeme ya msongo wa kilovolti 33 katika eneo la Morogoro ili kuruhusu ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400, ambao ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuimarisha miundombinu ya umeme nchini.
TANESCO imesema huduma ya umeme itasitishwa kila siku kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika maeneo yatakayoathirika, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha kazi zinafanyika kwa usalama na mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Maeneo yatakayokumbwa na kukosekana kwa umeme ni pamoja na Kiwanda cha Mkulazi, pamoja na Turiani inayohudumia maeneo mbalimbali ya wilaya za Mvomero, Kilosa, Kilindi na Gairo.
Katika Wilaya ya Mvomero, maeneo yatakayoathirika ni pamoja na Wami Sokoine, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Halmashauri ya Mvomero, Kituo cha SGR pamoja na kata za Dakawa, Mvomero, Kinda, Maskati, Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mhonda, Kweuma, Diongoya, Mtibwa, Kanga, Mziha, Pemba na Kibati.
Wilaya ya Kilosa itahusisha maeneo ya Dumila, Kitete, Ukaguru, Mfuru, Madudu, Mabana, Mateteni, Mbigiri na vijiji vya Tarafa ya Magole, huku Wilaya ya Kilindi ikiathiriwa katika baadhi ya vijiji ikiwemo Kikunde, Kwekivu, Ludewa, Tunguli, Namtoro na maeneo ya jirani. Pia baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Gairo vitakosa huduma ya umeme katika kipindi hicho.
Shirika hilo limewaomba wananchi na wateja wake kuwa na uvumilivu wakati wa utekelezaji wa kazi hizo, likisisitiza kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuboresha mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini.





