Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imepanda na kuvuka dola 90 kwa pipa, ikitoka katika kiwango cha takribani dola 70 ilichokuwa imefikia baada ya makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani. Ongezeko hilo limechochewa na kuongezeka kwa mvutano katika Mlango wa Hormuz, moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Hofu ya kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta imeongezeka baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) kudai kuwa meli mbili za mafuta zililipuka katika njia ya kusini ya Mlango wa Hormuz. Hata hivyo, jeshi la Marekani limepinga madai hayo na kuyataja kuwa si ya kweli, jambo linaloonyesha kuwa taarifa kuhusu tukio hilo bado zinapingwa.

Kupanda kwa bei ya mafuta kunatajwa kuwa pigo jipya kwa uchumi wa dunia kwa kuwa mafuta ni nguzo ya shughuli nyingi za kiuchumi. Wachambuzi wanasema ongezeko hilo linaweza kuongeza gharama za usafiri wa anga, baharini na barabarani, uzalishaji viwandani, kilimo, ujenzi, uchimbaji madini na usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, hali hiyo inaweza kuchochea mfumuko wa bei, kuongeza gharama za maisha na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi, hususan kwa nchi zinazotegemea kuagiza mafuta kutoka nje.

Mlango wa Hormuz hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani kwa njia ya bahari, hivyo tukio lolote la kiusalama katika eneo hilo huwa na athari kubwa kwa upatikanaji wa mafuta na mwenendo wa bei katika soko la dunia. Pia limeongeza taharuki kwa kampuni za usafirishaji wa mafuta, kampuni za bima na masoko ya fedha
Wataalamu wa sekta ya nishati wanaonya kuwa ikiwa mivutano kati ya Iran na Marekani itaendelea, upatikanaji wa mafuta unaweza kuzidi kupungua na bei ya Brent kuendelea kupanda katika siku zijazo.





