KIBAHA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amewataka wawekezaji katika sekta ya viwanda kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za mazingira ili kulinda mazingira na kuendeleza ajira kwa Watanzania.
Masauni alitoa wito huo Julai 20, 2026, wakati wa ziara ya kikazi mkoani Pwani, ambapo alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha, ikiwemo uwekaji wa jiwe la msingi katika kituo cha biashara kilichojengwa na halmashauri hiyo pamoja na shule mpya ya mchepuo wa Kiingereza katika Kata ya Kongwe.
Alisema Serikali haiwezi kufurahia kuona viwanda vikifungwa kwa sababu ya kukiuka sheria za mazingira, wakati vina nafasi ya kutoa ajira kwa vijana na kuchangia maendeleo ya uchumi.
“Tunahitaji uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu, lakini hatupendi uwekezaji unaokiuka sheria za mazingira. Wawekezaji waendelee kushirikiana na mamlaka husika ili miradi yao isiwe kero kwa wananchi,” alisema Masauni.
Alisisitiza kuwa kila mwekezaji ana wajibu wa kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria na kutoa manufaa kwa jamii inayowazunguka.
Masauni pia aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji unaoendelea Kibaha kwa kujiajiri na kuajiriwa, akisema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya biashara ili kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na uchumi.
Aidha, alisema Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji kutokana na ukaribu wake na Jiji la Dar es Salaam, huku miundombinu inayojengwa ikitarajiwa kuboresha huduma za biashara na usafirishaji, ikiwemo karakana ya kisasa itakayohudumia magari yanayopita katika barabara kuu ya Dar es Salaam kuelekea mikoa mingine.








