HomeHabariKiswahili chazidi kung’ara dunia, fursa zaongezeka

Kiswahili chazidi kung’ara dunia, fursa zaongezeka

Stockholm, Sweden: Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Swahiba Mndeme, amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutumia lugha ya Kiswahili kama fursa ya kiuchumi, akisema lugha hiyo imeendelea kuenea na kutumika katika mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika nchi anazozisimamia, Balozi Mndeme alisema Kiswahili kina nafasi kubwa ya kutoa fursa mbalimbali zikiwemo ukalimani, ualimu, uanzishaji wa vituo vya lugha pamoja na shughuli za muziki na burudani.

Alisema Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden utaendelea kutumia Kiswahili kama nyenzo ya kuunganisha Watanzania wanaoishi katika nchi hizo na kuhamasisha umuhimu wa kukiendeleza.

“Kuishi ugenini hakuna maana ya kuacha mila na utamaduni wetu. Tuna jukumu la kusimamia lugha yetu na kuwarithisha watoto wetu Kiswahili,” alisema Balozi Mndeme.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden, Dario Jovic, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha lugha na utamaduni.

Dario alisema Sweden itaendelea kutoa fursa kwa Kiswahili kufundishwa nchini humo ili kuongeza idadi ya watu wanaozungumza lugha hiyo.

“Tanzania ni mshirika wetu mkubwa wa maendeleo. Sisi kama Sweden tunaichukulia lugha ya Kiswahili kama sehemu ya mkakati wetu katika ushirikiano wa kiuchumi,” alisema.

Naye Kiongozi wa Mabalozi wa Afrika nchini Sweden, Balozi Diana Gashumba, amesema Kiswahili sasa ni lugha ya Afrika kwa ujumla, hivyo kuna umuhimu wa mataifa kuendelea kushirikiana katika kukiendeleza.

“Tushirikiane kuiendeleza lugha hii ili iweze kupiga hatua zaidi, kwani kwa sasa nchi nyingi za Afrika zinazungumza Kiswahili,” alisema.

Katika maadhimisho hayo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitumia jukwaa hilo kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, ikiwemo Kreta ya Ngorongoro na vivutio vingine vilivyopo katika eneo hilo.

Afisa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo anayeshughulikia masoko, Michael Makombe, alisema Kreta ya Ngorongoro ni miongoni mwa vivutio vya kipekee duniani kwa kuwa ni eneo lenye mfumo hai wa wanyamapori na makazi ya wanyama wakubwa wanaotambulika duniani.

Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden pia unasimamia masuala ya kidiplomasia katika nchi za Denmark, Norway, Lithuania, Ukraine, Finland, Iceland, Latvia na Estonia.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments