HomeBiasharaSerikali kushughulikia kero 15 za wafanyabiashara wa mifugo

Serikali kushughulikia kero 15 za wafanyabiashara wa mifugo

📌 Awahimiza kuimarisha umoja wao

📌 Aahidi kuziwasilisha hoja kwa wizara na taasisi husika


Daudi Nyingo – DAR ES SALAAM

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Kakurwa, amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mifugo nchini ili kuongeza tija katika sekta hiyo na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza Julai 19, 2026, katika kikao na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake kilichofanyika katika ukumbi wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Temeke, Dar es Salaam, Waziri Kakurwa alipokea hoja 15 zilizowasilishwa na Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE).

Alisema changamoto hizo hazihusu wafanyabiashara wa Temeke pekee, bali zinaakisi hali halisi ya sekta ya biashara ya mifugo katika maeneo mengi nchini.

“Nimepokea masuala 15 ambayo yanahitaji kujadiliwa, kuchambuliwa na kufikiwa maamuzi yatakayosaidia kupunguza changamoto, kuongeza tija katika biashara zenu na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika uchumi wa familia na taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa hoja hizo zitawasilishwa katika wizara na taasisi husika ili zipatiwe ufumbuzi, akibainisha kuwa Serikali ina dhamira ya kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo nchini.

Waziri Kakurwa pia aliwahimiza wafanyabiashara kuendelea kuimarisha umoja wao, akisema mshikamano ni nyenzo muhimu ya kutetea maslahi yao, kushiriki katika maboresho ya sera na sheria pamoja na kuongeza nguvu ya ushawishi kwa Serikali.

“Umoja ni nguvu. Kupitia umoja mnaweza kutetea maslahi yenu, kushiriki katika utungaji wa sera na kujenga sekta yenye nguvu zaidi,” alisisitiza.

Aidha, aliipongeza UWAMIMATE kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kikao hicho, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kujadili masuala yanayogusa sekta nzima badala ya maslahi ya kundi moja.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa UWAMIMATE, Joshua Lungwa, alisema umoja huo umeendelea kuwa jukwaa la kuwakutanisha wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake ili kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na Serikali.

Alisema kikao hicho kimewapa wafanyabiashara nafasi ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa Waziri na kupata ufafanuzi kuhusu hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa kuboresha mazingira ya biashara.

Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni ushuru wa mara mbili kwa ng’ombe wanaotoka mikoani, utitiri wa tozo, kuingia sokoni kwa mifugo isiyo na ubora, miundombinu duni ya minada, uuzaji holela wa nyama (besera), uwepo wa wafanyabiashara wasiotambulika kisheria (galagaja), changamoto za vibali vya uuzaji wa mifugo, faini kwa wainuaji wa mifugo, ukosefu wa soko la ngozi, hitaji la machinjio katika Wilaya ya Temeke, upatikanaji wa masoko ya nyama nje ya nchi, matumizi ya Power of Attorney kwa wainuaji wa mifugo, madai ya leseni ya uchinjaji katika eneo la Kibaha pamoja na changamoto za uongozi katika baadhi ya minada ya mifugo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments