HomeHabariProf Kabudi ataka mitambo ya Ubungo isimamiwe kwa ufanisi

Prof Kabudi ataka mitambo ya Ubungo isimamiwe kwa ufanisi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa ubunifu wa kununua mitambo ya ujenzi na matengenezo ya barabara, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha miundombinu, kuchochea shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa wananchi.

Prof. Kabudi alitoa pongezi hizo Julai 20, 2026, wakati wa uzinduzi wa mitambo ya malori ya Manispaa ya Ubungo itakayosaidia kuboresha mtandao wa barabara katika halmashauri hiyo.

Alisema uamuzi wa Baraza la Madiwani kuidhinisha ununuzi wa mitambo hiyo unaonyesha dira ya kutatua changamoto za miundombinu badala ya kutegemea uwezo wa taasisi nyingine pekee.

“Maamuzi haya si mepesi kufanywa na Baraza la Madiwani, kwa sababu yamelenga kutatua changamoto za barabara zinazowakabili wananchi. Ni muhimu mitambo hii isimamiwe vizuri ili ilete tija, na kila mtendaji aione ni mali ya wananchi inayopaswa kulindwa,” alisema Prof. Kabudi.

Aliongeza kuwa ubunifu huo unapaswa kuigwa na halmashauri nyingine nchini kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ili kuboresha huduma za miundombinu na kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mkoa huo umejipanga kuwekeza katika miradi yenye tija kwa wananchi badala ya kufikiria miradi midogo isiyoleta matokeo makubwa.

“Malengo yetu ni kutoka kwenye kuwaza mambo madogo na kuelekeza nguvu kwenye miradi mikubwa yenye manufaa kwa wananchi. Maendeleo lazima yawahusu wananchi na washiriki kikamilifu katika kuyajenga,” alisema Chalamila.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, alisema ununuzi wa mitambo hiyo umetokana na hitaji la kuboresha barabara zinazoharibika wakati wa mvua, hususan barabara za mitaani zinazotarajiwa kusimamiwa na TARURA.

Alisema wilaya hiyo ina mpango wa kuongeza uwekezaji kwa kununua seti nyingine ya mitambo ili kila jimbo liwe na uwezo wa kutekeleza kwa haraka kazi za ujenzi na ukarabati wa barabara, hatua itakayoboresha huduma za usafiri na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments