Mtwara: Naibu Waziri wa Michezo, Habari, Sanaa na Utamaduni, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya vijana kupitia michezo, elimu ya fedha na uwezeshaji wa kiuchumi.
Mwana FA ametoa pongezi hizo Julai 20, 2026, wakati wa kilele cha CRDB Bank Nanauka Festival, kilichohitimishwa na fainali za CRDB Bank Nanauka Cup zilizofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.
“Benki ya CRDB ni taasisi kubwa ya fedha. Inafurahisha kuona inawafikia vijana kupitia michezo na burudani. Leo tupo Mtwara kushuhudia fainali ya Nanauka Cup, lakini pia tunafahamu inafadhili mashindano mengine yanayowahusisha vijana. Hongereni sana Benki ya CRDB,” amesema Mwana FA.



Kutokana na kiwango kikubwa cha vipaji kilichoonekana katika mashindano hayo yaliyoanza Juni 13, Mwana FA amesema Mkoa wa Mtwara una hazina kubwa ya vipaji vya soka na kuwataka wadau kushirikiana kuhakikisha mkoa huo unapata uwakilishi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Mshindo Magimba, amesema mashindano hayo yaliyoshirikisha timu kutoka kata zote 18 za Jimbo la Mtwara Mjini yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuwafikia vijana kwa elimu ya fedha pamoja na fursa za kiuchumi.
“Benki ya CRDB tunaamini vijana ni nguvukazi muhimu ya maendeleo ya taifa. Ndiyo maana tunaendelea kuwafuata walipo na kuwekeza katika michezo, sanaa, ubunifu, ujasiriamali na uzalishaji ili kuwaunganisha na fursa za kujikwamua kiuchumi,” amesema Magimba.





Amebainisha kuwa hadi sasa Benki ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 15 kwa wajasiriamali wa sekta mbalimbali nchini, hatua iliyochangia kukuza biashara, kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi wa taifa.
Magimba amesema ushiriki wa benki hiyo katika maendeleo ya vijana unaonekana pia kupitia udhamini wa mashindano na programu mbalimbali, zikiwemo CRDB Bank Federation Cup, Imbeju-Ndondo Cup, CRDB Bank Taifa Cup, Zuchu-Imbeju Masterclass na CRDB Bank Bongo Star Search.
Katika fainali hizo, Naliendele FC iliibuka bingwa baada ya kuifunga Vigaeni FC mabao 3-0 na kutwaa kombe pamoja na kitita cha Shilingi milioni 3.
Mashindano hayo yanaandaliwa na Mbunge wa Mtwara Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa wananchi, kuibua vipaji na kutoa fursa ya kujadili maendeleo ya jimbo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nanauka ameishukuru Benki ya CRDB kwa kudhamini mashindano hayo, akisema udhamini huo umewezesha vijana kukutana, kuonyesha vipaji vyao na kujenga mshikamano kwa zaidi ya mwezi mmoja.





