Wadau wa mchezo wa kuogelea Tanzania wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya kiwango cha kimataifa kupitia programu ya wiki tatu iliyolenga kukuza vipaji vya waogeleaji vijana, kuimarisha uwezo wa makocha wazawa pamoja na kuwaelimisha wazazi kuhusu namna bora ya kuwaunga mkono wanamichezo katika safari yao ya mafanikio.
Programu hiyo iliyopewa jina la ‘Tanzania Performance Development Series 2026’, imeandaliwa na RaceBetter kwa ushirikiano na Monti AquaForce na itafanyika kuanzia Julai 28 hadi Agosti 14 katika Kampasi ya Mikocheni ya Shule ya Kimataifa ya Monti, jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yataongozwa na kocha mashuhuri wa kimataifa wa uogeleaji na mwanzilishi wa RaceBetter, Ben Lee, ambaye anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam Jumatatu kutokea nchini Marekani.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes, alisema mpango huo unaashiria mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu unaolenga kuimarisha maendeleo ya mchezo wa uogeleaji nchini Tanzania kwa kuunganisha utaalamu wa kimataifa na uongozi wa ndani ili kujenga mfumo endelevu wa kukuza vipaji kuanzia ngazi ya msingi hadi ushindani wa kiwango cha juu.
Mfululizo wa mafunzo hayo utaanza kwa Warsha ya Maendeleo ya Makocha itakayofanyika Julai 28 hadi 30, ikiwakutanisha makocha wa uogeleaji, walimu na viongozi wa vilabu vya uogeleaji.

Warsha hiyo inalenga kuboresha viwango vya ufundishaji huku ikiwapa makocha wa ndani fursa ya kujifunza na kufanya kazi bega kwa bega na Ben Lee katika kipindi chote cha kambi za mafunzo kwa wanamichezo.
Fatma alisema pia kutakuwa na kambi tatu za mafunzo kulingana na makundi ya umri wa washiri.
“Kambi kwa waogeleaji wenye umri wa miaka 6 hadi 8, itafanyika kuanzia Julai 30 hadi Agosti 1. Itafuatiwa na Kambi kwa waogeleaji wenye umri wa miaka 9 hadi 12 kuanzia Agosti 3 hadi 7.
Programu hiyo itahitimishwa na Kambi kwa waogeleaji wenye umri wa miaka 13 na kuendelea, itakayofanyika kuanzia Agosti 10 hadi 14.
Pia kutakuwa na mfululizo wa mafunzo kwa wazazi, yatakayotolewa bila malipo sambamba na kambi hizo. Vipindi hivyo vitajikita katika lishe na urejeshaji wa nguvu kwa wanamichezo, kujenga kujiamini na ustahimilivu, pamoja na kuwasaidia wazazi kujenga utaratibu mzuri wa maisha unaowawezesha watoto wao kufanikiwa ndani na nje ya bwawa la kuogelea,” alisema.




