KILIMANJARO: Serikali imehimiza sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi na kusafirisha mazao kwa mfumo wa ubaridi (Cold Chain) ili kupunguza upotevu baada ya mavuno, kulinda ubora wa bidhaa na kuongeza mauzo ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Mpita Msofe, na mwenzake wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbuasi, wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha kuhifadhi na kusafirisha mazao ya bustani kinachoendeshwa na kampuni ya Swissport katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Novemba 7, 2026.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za maandalizi ya Kongamano na Maonesho ya Horticulture Logistics Africa yanayofanyika Arusha, yanayolenga kuonesha fursa za uwekezaji na biashara katika sekta ya mazao ya bustani.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Profesa Msofe ameipongeza Swissport kwa kuwekeza katika kituo chenye uwezo wa kuhifadhi tani 180 za mboga na matunda. Amesema miundombinu hiyo ni muhimu katika kulinda ubora wa mazao kuanzia shambani hadi yanapowafikia walaji katika masoko ya nje.

Amesisitiza kuwa mfumo wa uhifadhi wa ubaridi unapaswa kujumuisha mnyororo mzima wa usafirishaji, kuanzia mashambani, vituo vya ukusanyaji na maghala, magari maalumu ya kusafirisha mazao hadi vituo vya mizigo katika viwanja vya ndege.
Amesema kwa mujibu wa taarifa za Swissport, kituo hicho hutumika kwa kiwango cha juu cha takribani asilimia 76, jambo linaloonesha kuwa bado kuna nafasi ya kuongeza matumizi yake kwa kuwahamasisha wakulima na wafanyabiashara kutumia huduma hizo kusafirisha mazao katika masoko ya kimataifa.
Pia ameipongeza kampuni ya Taha Fresh kwa kukusanya mazao kutoka kwa wakulima, kuyafikisha katika kituo hicho kwa ajili ya kuhifadhiwa na kuyaunganisha na masoko yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbuasi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Rajab Salum, ameipongeza Swissport, Taha Fresh na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana kuwezesha uwekezaji huo.

Amesema miundombinu ya uhifadhi wa ubaridi ina mchango mkubwa katika kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, hasa zile zilizoongezwa thamani kupitia uchakataji na usindikaji.
Ameeleza kuwa uwepo wa miundombinu hiyo unatoa fursa kwa viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo na mifugo kusafirisha bidhaa zao katika masoko ya kimataifa zikiwa katika hali inayokidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Akitolea mfano sekta ya nyama, amesema bila kuwa na miundombinu ya kutosha ya uhifadhi wa ubaridi, itakuwa vigumu kuongeza mauzo ya nyama iliyochakatwa, na hivyo nchi kuendelea kutegemea zaidi usafirishaji wa mifugo hai.
Amefafanua kuwa manufaa makuu ya miundombinu hiyo ni kulinda ubora wa bidhaa wakati wa usafirishaji na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Mbuasi amesema Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameelekeza Taasisi ya TanTrade kushirikiana na Taha pamoja na taasisi nyingine za Serikali kubaini fursa za uwekezaji katika miundombinu ya Cold Chain katika mikoa mbalimbali nchini.

Amesema lengo ni kujenga mfumo jumuishi wa uhifadhi na usafirishaji wa bidhaa, unaoanzia shambani, kupitia vituo vya ukusanyaji na uchakataji, kisha kusafirishwa hadi viwanja vya ndege kwa ajili ya kupelekwa katika masoko ya kimataifa.
Amewahimiza wawekezaji na wadau wa sekta binafsi kuwasiliana na TanTrade ili kupata taarifa za fursa zilizopo na kushiriki katika uwekezaji huo.
Akizungumzia usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, Mbuasi amesema Serikali inaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali kuhamasisha upatikanaji wa ndege za mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ili kuongeza uwezo wa kusafirisha bidhaa za Tanzania kwenda masoko ya nje.
Ameongeza kuwa aina ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinaendelea kubadilika, huku fursa za kusafirisha bidhaa zilizoongezwa thamani zikiongezeka kutokana na uwepo wa miundombinu inayowezesha kuzihifadhi katika ubora unaohitajika.
Kwa upande wake, Profesa Msofe amesema Wizara ya Kilimo inaendelea kutekeleza Ajenda ya Kilimo 10/30, inayolenga kuongeza mchango wa sekta hiyo katika mapato ya Taifa hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Amesema pia Serikali inatekeleza Mpango Kabambe wa Kilimo wa mwaka 2050, unaolenga kufikisha thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi katika dola za Marekani bilioni 100.
Ameeleza kuwa juhudi nyingine zinazotekelezwa ni kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora, mbolea, huduma za ugani kupitia Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) na miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Ziara hiyo pia imehusisha viongozi na watendaji kutoka mikoa mbalimbali yenye viwanja vya ndege, kwa lengo la kujifunza namna ya kutumia miundombinu hiyo kuboresha mazingira ya biashara na usafirishaji wa mazao ya wakulima.





