Makada 24, wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jana Agosti 12, 2025, wamechukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Kongwa, kufuatia kifo cha aliyekuwa Spika mstaafu na mbunge wa jimbo hilo Hayati Job Ndugai.

Chama hicho kilitangaza kuanza upya mchakato wa kuziba nafasi ya Hayati Ndugai, aliyeibuka kinara kwenye kura za maoni zilizopigwa na wajumbe Agosti 4, 2025 kwa kupata kura 5,690 na kuwashinda wengi tisa walipitishwa na vikao vya juu vya uteuzi wa chama hicho.
Katibu wa CCM, wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala, amesema jumla ya makada waliochukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho jana walikuwa ni 24 ambapo kati yao watatu ni wanawake.
“Waliochukua fomu leo (jana) walikuwa 24 ambapo kati yao watatu ni wanawake wanaume ni 21 na katika idadi hiyo wale wote tisa ambao walipishwa na Kamati Kuu ya CCM, Taifa pamoja na Hayati Spika mstaafu Ndugai wote wamechukua fomu lakini pia zipo sura mpya kumi kwenye idadi hiyo,”amesema Mkaugala
Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Kongwa kilitangaza kuanza upya mchakato wa kuchukua fomu za kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Kongwa Agosti 11, 2025,mara baada ya shughuli za maziko ya aliyekuwa Spika wa Bunge mstaafu na Mbunge wa jimbo hilo Hayati Job Ndugai.




