Serikali kupitia Mfuko wa SELF imepanga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 kwa kuwawezesha kiuchumi makundi mbalimbali katika jamii, kwa lengo la kuimarisha uchumi wa wananchi.
Mfuko huo wa serikali, ulioko chini ya Wizara ya Fedha na kuanzishwa mwaka 2015, tayari umeshawanufaisha wananchi 183,381, hasa wajasiriamali wadogo wakiwamo wanawake na vijana, kwa wastani wa asilimia 53.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko, Paul Sangawe, amesema tayari mfuko umeainisha vipaumbele vinane vya utekelezaji vitakavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 – 2050.
Aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa mfuko, serikali imetoa jumla ya Sh. bilioni 397 kwa wanufaika, ikiwamo wajasiriamali wanaojihusisha na biashara, kilimo na ufugaji, kwa lengo la kuwaongezea nguvu ya kujikwamua kiuchumi.
Kati ya vipaumbele vilivyowekwa, Sangawe ameitaja pamoja na: ufunguzi wa matawi mapya, uelimishaji wa jamii, ongezeko la mtaji, pamoja na uimara wa taasisi hiyo iliyo chini ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha.
Alisema pia kipaumbele kingine ni kufanya mapitio ya viwango vya riba ili ziwe rafiki zaidi kwa wananchi, kuongeza gawio kwa Serikali na kuimarisha ushirikiano wa wadau.
“Huduma za kifedha ni mojawapo ya kichocheo muhimu cha mageuzi ya kiuchumi Tanzania kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025/2050,” alisema Sangawe.
Aidha, Sangawe alibainisha kuwa uzinduzi wa Dira unaleta tafsiri ya mashirika na taasisi za umma kujipanga upya kwa kuzingatia malengo na vipaumbele vilivyowekwa, huku akisisitiza kuwa huu ni wakati wa kuendeleza jitihada ili kuhakikisha mfuko unaendelea kuhudumia wananchi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF, Santieli Yona, amesema jukumu kubwa la kwanza ni kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kuinuka kiuchumi. Pia, mfuko una jukumu la kutoa mikopo kwa taasisi za fedha zinazoendesha huduma za kifedha kwa wananchi katika ngazi za chini kabisa za jamii.
“Tuna jukumu kubwa la kujenga uwezo wa wajasiriamali kibiashara. Tangu tumeanzisha mfuko mwaka 2015, tumefanikiwa kutoa mikopo zaidi ya Sh. bilioni 397 kwa wananchi 183,381, sawa na asilimia 53, wakiwamo wanawake na vijana,” alisema Yona.