Thursday, March 5, 2026
spot_img
HomeHabariMiradi ya TACTIC ya bilioni 51 yainua miundombinu Arusha

Miradi ya TACTIC ya bilioni 51 yainua miundombinu Arusha

Mradi wa Uendelezaji wa Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) unatekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 51 katika Jiji la Arusha, ikilenga kuboresha miundombinu ya barabara, masoko na stendi za mabasi.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Arusha, Mhandisi Godfrey Bwire, alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 10.2, ikiwemo barabara ya Oljoro (Km 1.45), Olasiti (Km 3.96) na Ngoselotoni (Km 4.8). Alisema utekelezaji umefikia asilimia 72 na kugharimu shilingi bilioni 20.7.

Aidha, alisema TACTIC inajenga Soko jipya la Kilombero, Stendi ya kisasa ya Bondeni City kwa mabasi ya mikoani katika kata ya Murieti, na Soko jipya la nyama choma katika eneo la Kwa Mromboo. Miradi hiyo imefikia asilimia 6 na inagharimu shilingi bilioni 30.6.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. Maduhu Nindwa, alisema miradi hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa kutokana na mchango wake katika kukuza biashara na kutoa huduma muhimu. Alifafanua kuwa barabara mpya zitachochea upatikanaji wa huduma bora za elimu na afya.

“Kupitia barabara hizi, wanafunzi watasafirishwa kwa urahisi na kufika shuleni kwa wakati, hivyo kuongeza kiwango cha elimu. Pia zitasaidia mpango wa m-mama kwa kuwaondoa wajawazito na watoto kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na ucheleweshaji wa huduma za afya,” alisema Dkt. Nindwa.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Oloresho, James Stephano, alisema ujenzi wa barabara ya Oljoro umefufua biashara zilizokuwa zimeshuka kutokana na ubovu wa miundombinu, kwani wateja sasa wameanza kurejea.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments