Viongozi wa Kikristo mkoani Mwanza wamewahakikishia waumini na wananchi wote kuendelea kufurahia amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, huku wakisisitiza umuhimu wa kila mtu kutumia haki yake ya kupiga kura.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa makanisa, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa Mwanza, Askofu Josephat Magumba, alisema anaamini uchaguzi utafanyika kwa amani kwa kuwa taifa lipo mikononi mwa Mungu.
“Kanisa likisimama mbele, kila kitu kinaenda sawa. Tunaamini hakutakuwa na vurugu. Tutaendelea kuombea nchi na kuwafundisha watu wetu kulinda amani, rasilimali na uchumi wa taifa. Hivyo waumini wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa kuwa ni haki yao,” alisema Askofu Magumba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Mchungaji Lugayila Abel, alisema viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo ni jukumu lao kuhimiza amani na umoja hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.








