Katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zaidi ya watu milioni 940 bado hawana upatikanaji wa uhakika wa umeme, huku zaidi ya milioni 700 wakitegemea nishati hatarishi kama kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Nchini Tanzania, zaidi ya nusu ya wananchi — takribani watu milioni 36 — bado wanaishi bila umeme. Hali hii imekuwa ikisababisha familia nyingi vijijini kutegemea mafuta ya taa, mkaa na kuni kwa ajili ya mwanga na kupikia, jambo linalochangia changamoto za kiafya, kimazingira na kijamii.
Wanawake ndiyo wanaobeba mzigo mkubwa zaidi wa tatizo hili. Wengi hutumia muda mwingi kukusanya kuni, na kuvuta moshi wenye sumu wakati wa kupika, hali inayowaathiri kiafya na kuwanyima muda wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Puma Energy Foundation na Solar Sister Waja na Suluhisho




Ili kukabiliana na changamoto hizi, Puma Energy Foundation imeingia ubia na Solar Sister, shirika linalowawezesha wanawake kuanzisha biashara za kuuza taa na vifaa vya nishati safi katika jamii zao.
Tangu kuanzishwa mwaka 2010, Solar Sister imeunda mtandao wa zaidi ya wajasiriamali wanawake 12,000 waliowafikia watu zaidi ya milioni 5.5 katika nchi mbalimbali kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kupitia mpango huu, wanawake hupatiwa mafunzo ya masoko, uhasibu, mipango ya biashara, pamoja na ushauri na mikopo midogo.
Nchini Tanzania, mradi huu umewezesha zaidi ya watu milioni 2.3 kufikiwa na bidhaa za nishati safi tangu ulipoanzishwa mwaka 2013.
Awamu ya Kwanza Yazaa Matunda
Awamu ya kwanza ya ushirikiano wa Puma Energy Foundation na Solar Sister, iliyoanza mwaka 2023, ilijikita katika Mpango wa Kukuza Biashara.
Kupitia mpango huo, wanawake 579 walipatiwa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na mbinu za biashara. Uwezo huu umewasaidia kuongeza mauzo, kipato, na kufikia kaya nyingi zisizo na umeme kwa kutumia nishati safi.
Awamu ya Pili Kuendeleza Mafanikio
Awamu ya pili ya ushirikiano, iliyoanza mwaka 2025, inalenga kuajiri na kuwafundisha wanawake 500 zaidi katika mikoa mitatu mipya nchini Tanzania.
Pia, wanawake 200 wanapatiwa mafunzo ya biashara za kidijitali, huku bidhaa 16,000 za sola, ikiwemo majiko safi 2,000, zikitarajiwa kuuzwa vijijini.




“Lengo si kuuza bidhaa pekee, bali kuwawezesha wanawake kujiamini, kupata uhuru wa kifedha na heshima katika familia na jamii zao,”
alisema Cesear Mloka, Mkurugenzi Mkaazi wa Solar Sister Tanzania.
Hadithi za Mafanikio Zawapa Nuru Wanawake
Neema Ally, mkazi wa Songwe, aliwahi kufanya kazi ya kulima mashamba ya watu wengine kwa kipato kidogo. Baada ya kujiunga na Solar Sister, alianza biashara ya kuuza bidhaa za sola. Faida aliyopata ilimwezesha kukodisha ekari tano za ardhi na kuanzisha kilimo chake cha mahindi.
Leo hii, Neema anaendesha shamba lake, anaajiri wengine na anahakikisha watoto wake wanapata elimu bora.
Theresia John Robert, kutoka Kaskazini mwa Tanzania, alikuwa akipata riziki kwa kuponda mawe kwa mikono. Mwaka 2017 alijiunga na Solar Sister na kuanza kuuza taa za sola na majiko safi.
Kupitia kipato hicho, aliweza kujenga nyumba yake mwenyewe na kubadili kabisa maisha yake.
Hadithi zao ni mfano wa jinsi nishati safi inavyoweza kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi vijijini.
Kuelekea Maendeleo Endelevu
Kupitia ushirikiano huu, Solar Sister inalenga kuwafikia watu 85,000 nchini Tanzania kwa bidhaa za nishati jadidifu na salama, huku ikipunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuboresha afya za kaya vijijini.


“Tunajitahidi kuboresha maisha na kuleta mabadiliko yenye tija katika jamii,”
alisema Laura Fruehwald, Meneja wa Programu wa Puma Energy Foundation.
“Kupitia ushirikiano huu, nishati si tu chombo cha matumizi ya kila siku, bali kichocheo cha maendeleo endelevu.”
Puma Energy Yabeba Ajenda ya Nishati Safi
Nchini Tanzania, Puma Energy inaendeleza dhamira ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za nishati safi ya kupikia zilizo bora na nafuu.
Kupitia juhudi hizi, kampuni hiyo inasaidia ajenda ya kitaifa ya kupikia kwa nishati safi, kwa kutoa mbadala salama unaopatikana kwa urahisi kwa kaya nyingi.
Kwa kuunganisha nguvu za uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali na dhamira ya kutoa suluhisho la nishati safi, ushirikiano huu unaunda njia jumuishi ya maendeleo endelevu, ustawi wa jamii na maisha bora kwa Watanzania.







