Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia Chama cha Chaumma, Moza Ally amewaomba wananchi wa Kinondoni kumchagua ili akapiganie upatikanaji wa Katiba mpya bungeni.
Amesema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Kinondoni, zikiwa zimebaki siku mbili kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Nichagueni niende bungeni niende nikapiganie upatikanaji wa Katiba mpya. Nitakwenda kubanana na Waziri wa Katiba hadi kieleweke. Na wakinifukuza mjiandae kunipokea na nitazunguka nchi nzima kuipigania, alisema Moza.
Moza alisema mbali na kupigania upatikanaji wa Katiba mpya pia atahakikisha wananchi wa Kinondoni wanapata majisafi na salama pamoja na mikopo ya asilimia 10.




