HomeHabariBandari ya Kilwa yaanza kazi

Bandari ya Kilwa yaanza kazi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amesema Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo iliahidiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan iko katika hatua za mwisho za kukamilika na ipo tayari kuanza kutoa huduma, baada ya kufikia asilimia 99.99 ya ujenzi wake.

Akizungumza leo Juni 25, 2026 wilayani Kilwa mkoani Lindi wakati wa zoezi la majaribio ya mitambo na miundombinu ya bandari hiyo, Telack amesema hatua iliyosalia ni kuwasha na kuthibitisha utendaji wa baadhi ya mitambo.

Amesema majaribio yaliyofanyika ni pamoja na mitambo ya kuzalisha barafu yenye uwezo wa kuzalisha tani 100 kwa siku kwa kugandisha kwa nyuzi joto -3, hatua ambayo ameieleza kuwa ni ishara ya wazi kuwa bandari hiyo sasa iko tayari kuanza kazi.

“Hii ni ishara kuwa Bandari yetu iko tayari kuanza kazi. Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ameandika historia kwa kujenga bandari ya kwanza ya kisasa ya uvuvi nchini ambayo itafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi,” amesema Telack.

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea kwa vitendo ubora wa mitambo na miundombinu iliyojengwa, ikiwemo mitambo ya barafu, matanki ya kuhifadhia mafuta na vifaa vingine muhimu vya uendeshaji wa bandari.

Telack amesema ameridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika pamoja na ufanisi wa mitambo hiyo, huku akimpongeza Rais Samia kwa kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa usimamizi mzuri wa mradi huo hadi kufikia hatua ya ukamilishaji wake, na kuwataka wavuvi na wadau wa sekta ya uvuvi kujiandaa kunufaika na fursa zitakazotokana na bandari hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Kisaka Meena, amesema bandari hiyo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, uchakataji na thamani ya mazao ya uvuvi nchini.

Amefafanua kuwa mradi huo utasaidia kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kuwezesha uhifadhi bora, uchakataji wa kisasa na upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Miundombinu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi George Kwandu, amesema matokeo ya majaribio yanaonesha mitambo yote inafanya kazi kwa ufanisi na kukidhi viwango vilivyokusudiwa.

Amesema baada ya kukamilika kwa majaribio ya mwisho, bandari hiyo itaanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments