Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amekabidhi rasmi mtambo wa kuchakata na kusafisha maji ya chumvi ya kisima yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 125 kwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mburahati, ikiwa ni hatua ya Serikali kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Msando alisema kuwa mradi huo umetokana na ushirikiano kati yake na kamati hiyo pamoja na wadau wa maendeleo akisisitiza kuwa mitambo hiyo si ya kumilikishana bali ni kwa ajili ya kuhudumia wananchi na kupunguza kero ya maji inayowakabili mchana na usiku.
“Changamoto zipo kwenye kata na mitaa, na wanaoumia zaidi ni wananchi. Serikali imeamua kuwakabidhi wananchi kupitia kamati zao ili wasimamie na kulinda miradi yao,” alisema Msando





Alieleza kuwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ina jukumu la kusimamia miradi yote ya maendeleo ikiwemo maji, afya na elimu, akibainisha kuwa maji ni msingi wa maendeleo kwa kuwa yana uhusiano wa moja kwa moja na afya ya jamii.
”Maji ni maendeleo. Uwekezaji kwenye maji unaokoa gharama kubwa za matibabu kwa sababu magonjwa mengi hutokana na matumizi ya maji yasiyo salama,” aliongeza.
Katika hatua nyingine,Msando alitoa onyo kali kwa viongozi, vikundi na watu binafsi waliopokea mikopo ya halmashauri kupitia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kushindwa kurejesha, akisema Serikali haitavumilia tena tabia ya matumizi mabaya ya fedha za umma.



Kwa mujibu wa Msando, Halmashauri ya Ubungo ina jumla ya Sh. bilioni 14 za mikopo inayozunguka, lakini kiwango kilichorejeshwa ni kidogo, hali inayokwamisha utoaji wa mikopo kwa wananchi wengine wenye uhitaji.
“Uchaguzi umeisha. Aliyekopa lazima arejeshe. Fedha hizi ni za wananchi wote, si mali ya mtu au kikundi binafsi,” alisisitiza.




Aliwaagiza watendaji wa kata kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha vikundi vyote vinavyodaiwa vinatambuliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, huku fedha zitakazorejeshwa zikielekezwa kwenye kata ambazo hazikupata fursa ya mikopo kutokana na ucheleweshaji huo.
Msando alihitimisha kwa kuwataka wananchi na viongozi kushirikiana katika kulinda miradi ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa manufaa ya jamii nzima.








