Imeelezwa kuwa hali ngumu ya kiuchumi imewasababisha vijana wengi kukumbwa na msongo wa mawazo na kujikuta wakitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Wolfgang Pisa, kando ya Mkutano wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA), unaofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Mhashamu Pisa amesema hali hiyo pia inawasukuma vijana wengi kukumbwa na shinikizo la kuhama nchini kutafuta fursa katika maeneo mengine, jambo alilosema ni hatari ikiwa hawatatayarishwa vizuri.
Pisa, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, amesisitiza umuhimu wa kuzungumza na vijana mara kwa mara kupitia njia mbalimbali, ikiwamo mitandao ya kijamii, na kuwahamasisha kutumia mitandao hiyo kwa njia sahihi.
“Wengine ni wahanga wa mazingira kwa sababu ya uchumi, na moja ya matatizo makubwa ni mambo mawili. Kutokana na hizo changamoto, moja ni wanasiasa, wanasiasa wanaotumia vijana kufikisha malengo yao, lakini vijana kwa sababu hawana uchaguzi mkubwa katika uchumi, wakati mwingine ni aidha nijiunge au nitakufa njaa,” ameeleza Pisa.
Amesema kuna haja ya kuwaweka vijana hao karibu na kuwapa ushauri na maelekezo ili wasitumbukie katika tatizo hilo.




