Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka waajiriwa wake wapya kuzingatia weledi, nidhamu na maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa walipakodi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo, wakati akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya yanayofanyika katika Chuo cha Kodi, jijini Dar es Salaam.
Kayombo alisema mtumishi wa TRA anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, kuwaheshimu walipakodi na watumishi wenzake, huku akisisitiza kuwa nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio katika utendaji wa kazi.

Maadili, weledi, kuzingatia kanuni na taratibu za utumishi wao ni nguzo muhimu katika utendaji kazi ndani ya TRA na kutoa huduma bora kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla, alisema.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea waajiriwa wapya uelewa wa majukumu yao, maadili ya utumishi na utamaduni wa kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ili waanze majukumu yao kwa ufanisi.





