Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), Deogratias Mahinyila, ametoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali kushirikiana kuhakikisha hali ya matumizi ya tuhuma za ugaidi dhidi ya wananchi inakomeshwa, akidai kuwa imekuwa ikitumiwa kuwabambikia watu kesi na kulichafua taifa.
Akizungumza leo katika ofisi za zamani za CHADEMA zilizopo Ufipa, Dar es Salaam, Mahinyila amesema kuwa utaratibu wa kuwasingizia na kuwabambikia wananchi kesi za ugaidi hauna haki na unaweza kuharibu taswira ya Tanzania ndani na nje ya nchi.
Amedai kuwa kauli zinazotolewa kuhusu uwepo wa ugaidi nchini zinazua hofu miongoni mwa wananchi na zinaweza kudhoofisha uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine pamoja na kuathiri mazingira ya uwekezaji na utalii.
Mahinyila alisema taarifa zilizowahi kutolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 130 wanakabiliwa na tuhuma za ugaidi, akisisitiza kuwa hali hiyo si jambo la kawaida kwa taifa na inapaswa kutazamwa kwa umakini.
Amehoji mantiki ya kauli zinazodai kuwa Tanzania haina ugaidi wakati kuna watu wanaoshikiliwa na kushtakiwa kwa makosa hayo, akidai kuwa baadhi ya watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka yasiyo ya kweli.
Aidha, ameeleza kuwa matumizi ya kesi za ugaidi yanaweza kuwa na athari kwa taswira ya Tanzania kimataifa, akidai pia kuwa yanaweza kuathiri maandalizi ya michuano ya AFCON kutokana na umuhimu unaowekwa na vyombo vya michezo duniani katika masuala ya haki za binadamu.




