HomeBiasharaWRRB yaja na mikakati mitano ya kukuza mfumo wa stakabadhi za ghala

WRRB yaja na mikakati mitano ya kukuza mfumo wa stakabadhi za ghala

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetangaza maeneo matano ya kimkakati itakayoyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31, yenye lengo la kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, kupanua huduma zake na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Idara ya Habari – MAELEZO.

Amesema maeneo hayo ya kimkakati ni kupanua mfumo katika sekta mpya za uzalishaji, kuongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kuimarisha ushiriki wa taasisi za fedha, kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya maghala na huduma za biashara, pamoja na kuendelea kutoa elimu, kuutangaza na kuukuza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. 

Bangu amesema katika mkakati wa kupanua mfumo, WRRB itaanza kuingiza sekta ya mifugo katika Mfumo huo kuanzia mwaka wa fedha 2026/27, ambapo mnada wa kwanza wa mifugo kupitia mfumo huo unatarajiwa kufanyika Wilaya ya Mvomero.

Aidha, amesema bidhaa nyingine zikiwemo mwani, ngozi, mazao ya bustani na bidhaa nyingine zitakazokidhi vigezo zitaendelea kujumuishwa katika mfumo huo. 

Amesema WRRB pia itaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ikiwemo WRS-MIS, WRMS na matumizi ya stakabadhi za kielektroniki ili kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau wa mfumo. 

Kadhalika, amesema Bodi itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania, benki za biashara na taasisi nyingine za fedha ili kuongeza upatikanaji wa mikopo inayotumia stakabadhi za ghala kama dhamana. 

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Bangu amewahamasisha wawekezaji kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa maghala ya kisasa ili kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi bidhaa kwa usalama, kupunguza upotevu na kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa. 

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo utaongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika biashara, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza ajira, mapato ya Serikali na Halmashauri, pamoja na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia biashara yenye ushindani, uwazi na tija.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments