Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mohammed Ali Kawaida ametoa wito kwa Vijana kuendelea kujikusanya na kuwa na maandiko bora ili kuweza kupata mikopo inayotolewa na Serikali.
Amesema fedha hizo za mikopo zimetengwa kwa lengo la watu kunufaika ikiwemo vijana ili kuweza kupata mitaji ya kujiendeleza.
Aliyasema hayo jana Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake iliyoanza leo,Kawaida alisema kumekuwa na upotoshaji kutoka kwa baadhi ya wapinzani kuhusu unufaikaji wa miradi ya mikopo ya Serikali kuwa vijana hawapati mikopo hiyo.
Alisema jambo hilo linalosemwa na watu hao halina ukweli kwani mtaani vijana wananufaika ikiwemo vijana wa mkoa huo ambao wamenufaika na mkopo wa Shilingi 50 milioni kwa ajili ya kufyatua tofali.




“Hivi karibuni nimemsikia Mwenyekiti mmoja wa Chama kimoja yeye kila siku anaongea na Waandishi wa habari kazi yake kuinanga Wizara ya Vijana akisema hakuna kinachofanyika…nikasema mimi nipelekeni nikaone kwa ushahidi Serikali ya Dkt. Samia inachofanya, yeye anakwenda na makaratasi mimi nimekuja kushuhudia.
“Kiongozi wa Vijana cha Upinzani amekuwa anadanganya Watanzania kuwa hawapati mikopo bila ushahidi wa kwenda kujionea wangekuja kama mimi wajionee Vijana wanavyonufaika na Mikopo ya Serikali na kuacha kupotosha umma,”alisema
Aidha Kawaida alisema ziara yake katika Mkoa wa Mtwara itagusa wilaya zote na lengo kuu litakuwa kuwaangalia watendaji wazembe wanaokwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025-2030.
Alisema hatakuwa na huruma na watendaji wazembe kwani Wananchi wameiamini Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na haiwezekani wachache kuikwamisha.
“Kwa lugha nyepesi naweza kusema nimekuja kukagua Ilani ya Chama cha Mapinduzi mkoani Mtwara ila kwa lugha ngumu ni kuwa nimekuja kushughulika na Watendaji wazembe wa Ilani yetu ya CCM,” alisema Kawaida








