Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Iddy Msuya, amekutana na wenyeviti wa vitongoji tisa vya Mji Mdogo wa Usa River kujadili changamoto za huduma ya maji na kuweka mikakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Kikao hicho kilifanyika chini ya uenyekiti wa Diwani wa Kata ya Usa River, Daud Mkuba, na kilihudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, Kamati ya Siasa ya Kata, viongozi wa vitongoji pamoja na watendaji wa AUWSA.
Mkuba alimpongeza Mhandisi Msuya kwa kuaminiwa na Serikali na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Arusha, huku akiishukuru mamlaka hiyo kwa juhudi zinazoendelea kufanywa kuboresha huduma ya maji katika kata hiyo.


Katika majadiliano, viongozi wa vitongoji waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, zikiwemo uchakavu wa miundombinu unaosababisha mivujo ya maji, kuchelewa kuzibwa kwa mivujo, ucheleweshaji wa maunganisho mapya ya maji, mabomba yaliyowekwa kutounganishwa kwa kukosekana kwa baadhi ya vifaa na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu huduma za maji na usomaji wa mita.
Akijibu hoja hizo, Mhandisi Msuya alisema AUWSA imejipanga kuboresha huduma ya maji kupitia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ununuzi wa mita mpya za maji.
”Kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mita za maji, lakini katika mwaka wa fedha 2026/2027 AUWSA inatarajia kununua mita za maji 40,000. Hatua hii itaondoa kwa kiasi kikubwa changamoto ya kuchelewa kuwaunganishia wananchi huduma ya maji,” alisema.

Aidha, aliagiza watendaji wa AUWSA kushughulikia kwa haraka changamoto zinazoweza kutatuliwa mara moja, hususan kuziba mivujo ya maji, kuharakisha maunganisho mapya na kuunganisha mabomba yaliyokwishalazwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo bila kuchelewa.
Mhandisi Msuya pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kulipia huduma za maji kwa wakati ili kuiwezesha AUWSA kuwekeza zaidi katika kuboresha miundombinu na kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika, endelevu na yenye ubora.
Kwa upande wao, viongozi wa vitongoji walieleza kuwa wananchi wako tayari kuunga mkono maboresho ya tozo za huduma ya maji endapo yataambatana na uwekezaji zaidi katika miundombinu na kuboresha huduma.







