Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeanza uchunguzi wa tukio la kuvunjwa kwa ukuta na kuibwa kwa matofali katika eneo linalodaiwa kuwa la mmiliki halali, lililopo Kijiji cha Udindivu, Kata ya Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea Julai 18, 2026 ambapo mmiliki wa eneo hilo, Jumanne Tindi, ambaye alikuwa mkoani Kilimanjaro, alipokea taarifa kutoka kwa msimamizi wa eneo lake, Rajabu Tindi, kuwa ukuta wa kiwanja chake ulikuwa umevunjwa na matofali kuibwa.
Mmiliki huyo anadaiwa kuwa na kiwanja namba 417, Block K, Mapinga, chenye ukubwa wa mita za mraba 942, ambapo alijenga ukuta wa kuzunguka eneo hilo tangu mwaka 2016.
Baada ya kupata taarifa hiyo, Jumanne Tindi alimjulisha Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanja vya Mapinga Satellite City, Mchata Michael, ambaye baadaye alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mapinga kuhusu tukio la uharibifu wa mali na wizi wa matofali.
Polisi ilieleza kuwa kutokana na kutokuwepo kwa mmiliki wa eneo hilo au ndugu yake wa karibu, ukaguzi wa awali wa eneo la tukio ulisubiri hadi taratibu muhimu zikamilike.
Tarehe 21 Julai 2026, Mchata Michael aliwasiliana na Rajabu Tindi ili kufika Kituo cha Polisi Mapinga kwa ajili ya kufungua kesi ya uharibifu wa mali, ambapo hatua hiyo iliambatana na ukaguzi wa eneo la tukio.
Ukaguzi huo uliongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani pamoja na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.
Wakati timu ya Polisi ikiwa eneo hilo ikifanya ukaguzi ili kubaini hali ya uharibifu, baadhi ya watu waliodaiwa kuwa wavamizi walijitokeza na kujaribu kuzuia zoezi hilo kwa kuitana kupitia kipaza sauti.
Hata hivyo, Polisi ilisema ukaguzi ulikamilika bila tatizo na timu hiyo iliondoka eneo hilo salama.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeeleza kuwa linaendelea na taratibu za kisheria kwa lengo la kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha hatua za uchunguzi watuhumiwa wa tukio hilo.
Aidha, Polisi limetoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria na taratibu za umiliki wa ardhi ili kuepuka migogoro inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.




