QNET imejitenga na madai ya udanganyifu yanayofanywa na watu wanaodai kuwa na uhusiano nayo nchini Tanzania, ikiwemo utapeli wa ajira.
Katika taarifa yake, kampuni hiyo imesisitiza kuwa haihusiki kwa namna yoyote na vitendo vya udanganyifu, na haishirikiani na mtu au kikundi kinachotumia jina lake kufanya shughuli zisizo halali kama kuomba malipo kwa ahadi za ajira au safari za nje ya nchi.
QNET imeeleza kuwa haiajiri wafanyakazi kupitia mfumo huo, bali inafanya kazi na Wasambazaji Huru (Independent Distributors – IDs) ambao ni wajasiriamali wanaopata kipato kupitia mauzo ya bidhaa, si ajira rasmi.
Aidha, kampuni imepiga marufuku vitendo vya kuwasilisha biashara yake kama ajira, kukusanya fedha zisizoidhinishwa, au kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu mapato na bidhaa zake.
QNET imezipongeza mamlaka za Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na matapeli na kueleza utayari wake wa kushirikiana na vyombo vya dola ili kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Wananchi wamehimizwa kuwa makini, kuthibitisha taarifa kupitia njia rasmi za kampuni na kuripoti vitendo vya kutiliwa shaka.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, inaendelea kuwekeza katika elimu kwa jamii na wasambazaji wake ili kuhakikisha biashara inafanyika kwa uadilifu na kwa kuzingatia maadili.
Ilianzishwa mwaka 1998, QNET ni kampuni ya kimataifa inayojikita katika bidhaa za mtindo wa maisha na ustawi, ikitumia mfumo wa biashara ya mtandaoni, huku ikilenga kuwawezesha wajasiriamali wadogo kujenga kipato chao.




