HomeBiasharaTRA yawapiga msasa wahasibu mabadiliko ya Sheria za Kodi 2026/27

TRA yawapiga msasa wahasibu mabadiliko ya Sheria za Kodi 2026/27

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewapatia Wahasibu  elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa masuala ya kodi kwa Wahasibu.

Akizungumza katika semina ya utoaji elimu ya mabadiliko ya Sheria za kodi 2026/27 kwa Wahasibu, Afisa Mwandamizi Msimamizi wa Kodi, Alex Mwambenja, amesema wahasibu ni wadau muhimu katika mfumo wa kodi kwa kuwa wanahusika moja kwa moja na usimamizi wa taarifa za kifedha za walipakodi.

Amesema kupitia semina hiyo, wahasibu hao wamepata fursa ya kufahamu mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika sheria za kodi pamoja na namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Aidha, elimu hiyo itawawezesha kuwashauri wateja wao kwa usahihi na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati.

“Tunatarajia elimu hii itawasaidia wahasibu kuwasimamia vizuri walipakodi wao na kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria. Pia tumepata nafasi ya kusikiliza changamoto mbalimbali walizozieleza ili tuweze kuzifanyia kazi na kuboresha utoaji wa huduma zetu,” ameeleza  Mwambenja

Amesema kuwa TRA inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa walipakodi kupitia utoaji wa elimu na maboresho ya mifumo mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Ameongeza kuwa semina hiyo ni ya kwanza kufanyika kwa mwaka huu kwa kundi la wahasibu, huku TRA ikitarajia kuendelea kutoa elimu kwa makundi mengine ya wataalamu ikiwemo washauri wa kodi pamoja na wadau wengine katika mikoa mbalimbali nchini.

“Lengo letu ni kuhakikisha elimu ya kodi hususani mabadiliko ya sheria za kodi inawafikia wadau wengi zaidi ili kila mmoja afahamu wajibu wake na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa kupitia ulipaji wa kodi,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mwambenja ameeleza kuwa TRA imeweka utaratibu wa kuwapa nafuu wafanyabiashara wapya ili kuwahamasisha kuingia katika mfumo rasmi wa kodi.

Amesema mfanyabiashara mpya mwenye mauzo ya kati ya Shilingi  moja hadi shilingi milioni 200 kwa mwaka atapatiwa msamaha wa kulipa kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanze shughuli zake.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments