๐ Dodoma
Ujumbe kutoka Zambia ukiongozwa na Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Matthews Jerre, umesema umevutiwa na maendeleo makubwa ya sekta ya madini nchini Tanzania, hususan namna shughuli za uchimbaji, mifumo ya masoko na vituo vya ununuzi vinavyoendeshwa kuanzia ngazi ya wachimbaji wadogo hadi wakubwa pamoja na sera thabiti inayosimamia rasilimali hizo.
Akizungumza Novemba 20, 2025 baada ya kupokea wasilisho maalum kuhusu mwenendo wa uchimbaji, usimamizi, masoko, sheria na taratibu za uwekezaji chini ya Sera ya Madini ya 2009, Balozi Jerre alisema Tanzania imeweka mifumo ya mfano inayostahili kuigwa barani Afrika.
Zambia yavutiwa na mifumo ya masoko ya madini Tanzania
Tisa Chama, Afisa Fundi Mkuu kutoka Kampuni ya Umma ya Zambia ya ZCCM-IH, alipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha mifumo imara inayounganisha masoko yote ya madini na vituo vya ununuzi, akisema Zambia inahitaji kujifunza ili kuweza kufahamu kwa uhalisia kiwango cha dhahabu kinachozalishwa nchini humo.




Naye Kennedy Mwandama, Afisa Biashara Mkuu wa ZCCM-IH, alisema amevutiwa na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya masoko ya madini, ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo katika utafiti na uchenjuaji, pamoja na miongozo inayowezesha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
โBinafsi nimevutiwa sana na matumizi ya teknolojia katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini. Hii ni hatua kubwa na ya manufaa kwa taifa,โ alisema Mwandama.
Tanzania yarasimisha mchango wa wachimbaji wadogo
Kamishna Msaidizi wa Madini, Archard Kalugendo, aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali iliamua kurasimisha sekta ya wachimbaji wadogo kutokana na mchango wao mkubwa ambapo hadi sasa wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini. Aidha, mwaka 2024 sekta hiyo ilichangia asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa.




Alisema mageuzi makubwa katika sekta ya madini yalianza baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya 2017, yaliyowezesha kuanzishwa kwa masoko rasmi na vituo vya ununuzi vya madini nchi nzima.
Kalugendo aliupongeza ujumbe huo kwa kutambua changamoto zao na kuchagua kuja Tanzania kujifunza mbinu bora za usimamizi wa dhahabu.
Ujumbe wa Zambia watembelea kiwanda cha Eyes of Africa
Mbali na wasilisho hilo, ujumbe huo ulitembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Eyes of Africa kilichopo Dodoma ili kujionea matumizi ya teknolojia katika usafishaji wa madini.
Mmiliki wa kiwanda hicho, Ference Molnar, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa viwanda vya kusafisha dhahabu, hususan katika ushirikiano na wachimbaji wadogo na taasisi za kifedha ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).







