Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na viongozi wa dini zote – Wakristo na Waislamu – imesisitiza kuwa amani ndiyo silaha muhimu ya kudumisha utulivu wa nchi, hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Katika tamko lao rasmi lililosomwa leo wakati wa Kongamano la Amani la Viongozi wa Dini Mbalimbali, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Charles Sekelwa, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa uhuru, haki na utulivu, ili kuchagua viongozi wanaofaa kuijenga Tanzania katika misingi ya amani, upendo na maendeleo.
“Baada ya kumaliza zoezi la kupiga kura, wananchi wanapaswa kurejea majumbani kwao kwa utulivu bila vurugu au maneno ya chuki, ili kudumisha taswira njema ya taifa,” alisema Sekelwa.

Ameongeza kuwa Kamati hiyo itaendelea kufanya sala, dua na maombi kumuomba Mungu aibariki Tanzania na kuendelea kuilinda katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya hapo.
Sekelwa alisisitiza kuwa amani ni nguzo ya maendeleo, umoja ni nguvu, na upendo ni suluhisho la changamoto zote, huku akiwataka Watanzania kuwaombea viongozi wa uchaguzi ili watekeleze majukumu yao kwa hekima na uadilifu.
Viongozi wa Dini Watoa Wito wa Amani
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, aliwataka wakazi wa mkoa huo kudumisha amani na kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura.
“Amani itasaidia taifa kuvuka salama kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi. Ni muhimu kuchagua viongozi sahihi watakaodumisha amani na maendeleo,” alisema Sheikh Kabeke.

Naye Charles Sekelwa aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchagua kwa kuzingatia sera za wagombea na kuepuka kushawishiwa kutojihusisha na uchaguzi.
“Oktoba 29, tutoke kwa wingi kupiga kura. Tusiachwe na maneno ya kukata tamaa au kuharibu kura. Kura yako ni sauti yako,” alisisitiza.

Upendo Isaya, mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, alisema kila Mtanzania mwenye amani ya moyo atafanya maamuzi ya busara, hivyo aliwataka wenye umri wa kupiga kura kujitokeza na kutumia haki yao ya kikatiba.
Viongozi wa Serikali Watoa Wito wa Utulivu
Waziri Mstaafu Lazaro Nyalandu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kushikamana na kuliombea taifa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alibainisha kuwa hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari na serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu.
“Serikali ipo kazini. Tumejipanga kulinda raia na mali zao na kuhakikisha nchi inaingia na kumaliza mchakato wa uchaguzi kwa amani na usalama,” alisema Mtanda.




